Mama Mariam aelezea utekelezaji maazimio ya Beijing
MKE wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi, jana amehutubia kikao cha ‘Building on Beijing’ na kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya, mageuzi ya sheria, uwezeshaji wa kiuchumi na maamuzi nchini Tanzania na Zanzibar katika kipindi cha miaka 30 ya maazimio hayo.
Mama Mariam alieleza hayo katika siku ya pili ya muendelezo wa mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Wake wa Marais wa Afrika (OAFLAD) ukumbi wa Umoja wa Afrika , Addis Ababa, Ethiopia.
Alieleza kuwa chini ya uongozi wake, taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) inaendelea kutekeleza ahadi za tamko la Beijing, ikiwawezesha zaidi ya wakulima wa mwani 1,690, kwa lengo la kufikia 5,000 ifikapo mwaka 2030.
Katika sekta ya afya ya uzazi alieleza wasichana 8,600 wamenufaika msaada wa taula za kufua, kupunguza uhaba wa taulo za hedhi na utoro shuleni huku taasisi hiyo ikifikia wanufaika zaidi ya 17,200 katika eneo la kuzuia utapiamlo, vifo vya akina mama na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Vilevile, alieleza kuwa mfumo wa Usimamizi wa Kesi za udhalilishaji (GBV) Zanzibar unaleta mabadiliko makubwa katika ufuatiliaji na usimamizi wa kesi za ukatili wa kijinsia.
Kwa upande mwingine Mama Mariam alieleza kuwa anaendelea kujitoa kuimarisha uongozi wa wanawake, kulinda urithi wa kiafrika na kusukuma mbele maendeleo endelevu.
Comments
Post a Comment