Maonesho ya magari yalivyovutia wadau Dom
NA MWANDISHI WETU, DODOMA
MAONESHO ya magari chapa ya Isuzu yaliyoandaliwa na kampuni ya Al Mansour Auto EA Tanzania, yamemalizika huku wadau wakiwemo Wabunge wakisema kufanyika kwake kumewaongezea uelewa kukabili changamoto za usafiri.
MBUNGE wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba (kushoto) akimsikiliza Ofisa Mauzo Mwandamizi wa kampuni ya Al Mansour Auto EA Tanzania inayouza na kusambazaji magari aina ya ISUZU nchini, Filbert Massawe, alipotembelea maonesho ya magari yaliyomAlizika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.
Akizungumza maonesho hayo yaliyokuwa yakifanyika katika viunga vya Akachube Plaza, jijini Dodoma, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Anurup Chatterjee, alieleza kuwa yalikuwa na mafanikio makubwa huku yakionesha kuwavutia na wadau wa sekta ya uchukuzi nchini.
Alisisitiza kuwa umuhimu wa maonesho hayo unatokana na kuangazia teknolojia za kisasa za usafiri wa magari ya Isuzu pamoja na kujenga uelewa wa washiriki kuhusu bidhaa mpya zilizoandaliwa kukidhi mahitaji tofauti ya usafiri nchini.
“Katika siku hizo tatu, tulifurahi kuonesha magari ambayo sio tu yana nguvu na kuaminika bali pia yametengenezwa kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji kutoka sekta mbali mbali”, alieleza Chatterjee.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yalikuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za serikali, wawakilishi wa kampuni za usafirishaji na wateja binafsi kuchunguza suluhisho za kisasa za magari zinazokusudia kubadilisha mazingira ya usafiri na usafirishaji.
Aidha Chatterjee alizishukuru mamlaka za serikali na uongozi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupokea onesho hilo lililohusisha aina zote za magari chapa ya Isuzu.
"Tunamshukuru sana Spika wa Bunge kwa kuhamasisha wabunge watembelee maonesho haya yaliyokuwa na magari kuanzia malori, mabasi makubwa hadi magari madogo (SUV) na pick-up ikiwa ni pamoja na modeli za Isuzu D-MAX zilizoongeza mvuto wa tukio hilo”, alieleza Chatterjee.
Aliongeza kuwa kupitia tukio hilo, walipata fursa ya kuona jinsi magari hayo yalivyoundwa mahsusi kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya umma, usafiri wa kilimo, operesheni za usalama na huduma muhimu katika sekta ya afya na elimu.
Maonesho hayo yalivuta umakini kutoka kwa baadhi ya Wabunge na viongozi waandamizi wa mashirikia na taasisi za serikali akiwemo Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba, aliyeonesha kuvutiwa na tukio hilo na kueleza kuwa maonessho hayo ni fursa muhimu kwa wadau wa usafiri na usafirishaji.
“Maonesho haya yamefungua macho yetu juu ya teknolojia za kisasa zinazopatikana katika sekta ya usafiri. Ninawashukuru waandaaji kwa kuonesha kujitolea kwa Isuzu katika kuipatia jamii magari bora na uaminifu unaoendana na dhamira yetu”, alieleza Kishimba.
Aidha aliishauri serikali katika kuboresha usafiri wa umma na kuendeleza miundombinu nchini kote kutumia kampuni hiyo ili kupunguza gharama wanapotafuta Suluhu za usafirishaji kwa taasisi zake.
Naye mdau wa sekta ya utalii jijini Dodoma, Elibariki Lekule (pichani kushoto), alisema, maonesho haya yamekidhi matarajio yake kwa kuwa kulikuwa na matoleo tofauti ya gari za ISUZU lilitoa fursa ya kufanya uchaguzi bora kulingana na mahitaji ya kibiashara na hivyo kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa wateja wao.
Naye, Meneja Mauzo na Masoko ya Nje Isuzu Afrika Mashariki, Bi. Sandra Njagi, pia alitoa shukurani zake za dhati kwa serikali ya Tanzania kwa ushirikiano thabiti kwa magari ya ISUZU. “Tumejizatiti kuandaa maonyesho kama haya mara kwa mara ili kuimarisha uhusiano na washirika wetu wa serikali na kudumisha mazungumzo ya wazi kuhusu kuendeleza sekta ya usafiri nchini Tanzania.”
Comments
Post a Comment