IPA tanuri la kuimarisha utumishi wa umma Z'bar

NA MWANAJUMA SAID, IPA

KATIKA kuimarisha mifumo ya utoaji huduma serikalini, hakuna jambo muhimu kama kuwa na watumishi wa umma wenye uwezo, maarifa na maadili ya kazi.

WAZIRI wa Nchi (AR) Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora, Dk. Haroun Ali Suleiman, akizungumza na uongozi wa Chuo cha Serikali cha Kenya waliofika ofisini kwake Mazizini  kwa ajili ya kujitambulisha.

Kwa kuliona hilo   Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nguvu kazi ya taifa inaimarishwa kupitia mafunzo ya kitaaluma na kiutendaji.

Chuo hicho kilichoanzishwa kwa sheria namba moja ya mwaka 2007 ni taasisi ya kiserikali ambayo iko chini ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora.

Miongoni mwa majukumu ya chuo hiki ni kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi.

Pamoja na kutoa programu za muda mrefu, IPA inatambulika kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi yenye kugusa maeneo mahsusi ya utendaji  kazi serikalini na kufanya tafiti na ushauri elekezi kwa watumishi wa umma na taasisi binafsi.

Tangu kuanzishwa kwake, IPA imekuwa nguzo muhimu ya kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na uadilifu katika sekta ya umma Zanzibar chini ya dhamira na Maono yake yanayolenga kuwa taasisi bora ya mafunzo ya utawala wa umma kwa maendeleo endelevu ya rasilimali watu Zanzibar.

MKUU wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), Dk. Shaaban Mwinchum Suleiman (kushoto) na Mkurugenzi mkuu wa Chuo cha Serikali cha Kenya, Professa Nura Mohamed wakisaini makubaliano ya ushirikiano katika utoaji wa mafunzo na tafiti kwa watumishi.

Aidha kupitia mitaala inayolenga matokeo na kufundishwa na wakufunzi wenye uzoefu, chuo kinachangia kwa kiwango kikubwa katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na watumishi wa umma wenye uwezo na taaluma ya hali ya juu.

Akizungumzia kuhusu dhamira na maono hayo, Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Shaaban Mwinchum Suleiman, alisema kuwa chuo kimejipanga kuhakikisha kinawafikia watumishi wengi zaidi ili kuwawezesha kupata taaluma bora na yenye viwango vya juu.

Dk. Shaaban alieleza kuwa moja ya malengo makuu ya chuo ni kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa umma kupitia utoaji wa mafunzo endelevu yanayolenga kuongeza ufanisi, uwajibikaji na uadilifu katika sekta ya umma.

Kwa kufanya hivyo, chuo kina mchango mkubwa katika maendeleo ya rasilimali watu na kuimarisha utawala bora nchini kupitia mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu”, alieleza Dk. Shaaban.

MAFUNZO YA MUDA MFUPI, MUDA MREFU

Katika kukabiliana na mahitaji ya haraka ya kitaaluma na kiutendaji kwa watumishi wa umma, Dk. Shaaban alileleza kuwa IPA inendelea kutoa  mafunzo ya muda mfupi  yaliyojikita katika maeneo matatu makuu.

Maeneo hayo ni mafunzo ya kustaafu yanayolenga kuwaandaa watumishi wanaokaribia au waliokwisha kustaafu, kwa maisha baada ya utumishi.

Mafunzo haya huwajengea washiriki uwezo wa kusimamia fedha zao kwa ufanisi baada ya ajira, kujihusisha na ujasiriamali wa maana, kujitunza kiafya na kisaikolojia na kujiandaa kifikra kwa mabadiliko ya maisha ya kustaafu”, alieleza Dk. Shaaban.

Aliongeza kuwa; “Kustaafu ni sehemu muhimu ya mzunguko wa maisha ya kila mtu. Wastaafu watarajiwa wanahitaji maandalizi ya kina ili waweze kuishi maisha bora, yenye furaha na manufaa kwao na jamii kwa ujumla.

MAFUNZO YA AWALI KWA WATUMISHI WAPYA

Kwa upande wa mafunzo ya awali kwa watumishi wapya, Dk. Shaaban alieleza kuwa watumishi wanaojiunga na utumishi wa umma hulazimika kupitia mafunzo hayo yanayowasaidia kuelewa mfumo wa serikali na taratibu za kiutumishi, kujifunza maadili ya kazi, uadilifu na uwajibikaji na kuelewa majukumu yao na namna ya kuwahudumia wananchi kwa weledi.

Alitaja malengo mengine kuwa ni kuwajengea misingi ya nidhamu ya kazi na mawasiliano ya kikazi watumishi, kufahamu vizuri suala la uzalendo wa nchi yao,kujua sheria na kanuni za utumishi ili kufanya kazi kwa kufahamu misingi yake.

Kupitia mafunzo haya, IPA huweka msingi imara kwa kizazi kipya cha watumishi wa umma”, aliongeza.

WATUMISHI wa umma wapya kutoka taasisi na idara mbali mbali za serikali wakishiriki mafunzo ya awali yanayotolewa na Chuo cha Utawala wa Umma (IPA).

MAFUNZO KWA WATUMISHI WALIOPO KAZINI 

Akizungumzia mafunzo ya kujenga uwezo kwa watumishi waliopo kazini, mkuu huyo wa chuo alilitaja kuwa ni hilo ni eneo muhimu linalowalenga watumishi walioko kazini kwa lengo la kuwapa maarifa mapya na kurahisisha  nafasi  zao kulingana na mabadiliko ya sera, teknolojia na mahitaji ya jamii.

Mafunzo haya hujumuisha usimamizi wa rasilimali watu na fedha, uongozi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, huduma kwa wateja na utatuzi wa migogoro na utumiaji wa TEHAMA katika utendaji wa kazi”, alifafanua Dk. Shaaban.

WATUMISHI wa umma wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakipatiwa mafunzo ya kujenga uwezo na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA).

Aliongeza kuwa IPA pia hutoa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa mawizara na taasisi za umma na maeneo mbali mbali ambayo huonekana na changamoto ya utendaji ambapo kupitia programu hizo watumishi wa umma huwezeshwa kuwa wabunifu, wenye tija na watoa huduma bora kwa umma.

CHANGAMOTO ZA IPA

Akizungumzia changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, Dk. Shaaban alieleza kuwa katika dunia inayobadilika kwa kasi, uimarishaji wa ujuzi na maarifa kwa watumishi wa umma ni jambo lisilozuilika. Alisema; “Mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi si tu yanawaongezea maarifa, bali pia yanaimarisha utendaji kazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, alieleza kuwa pamoja na umuhimu huo, bado kuna changamoto kubwa zinazokwamisha jitihada hizo ikiwemo ya baadhi ya taasisi kutotoa kipaumbele stahiki kwa mafunzo ya watumishi wao.


WASTAAFU watarajiwa kutoka katika wizara, idara na taasisi mbali za serikali wakipatiwa mafunzo elekezi kwa lengo la kujiandaa kukabiliana na maisha baada ya kustaafu.

Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Mafupi, Utafiti na Ushauri Elekezi, Mwalimu Abdallah Juma Ramadhan, alieleza kuwa  baadhi ya taasisi bado hazijatoa kipaumbele stahiki kwa suala la mafunzo kwa watumishi waowakiwemo wale wanaotarajiwa kustaafu.

Hali hii inasababisha watumishi wengi kukosa fursa muhimu za kushiriki kwenye mafunzo yanayoweza kubadili kwa kiasi kikubwa namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku”, alisema Mwalim Abdallah.

Aliongeza kuwa kwa kiasi kikubwa, mafunzo ni chachu ya mabadiliko na maendeleo ya kweli ndani ya taasisi yoyote. Kupitia mafunzo, watumishi huweza kuendana na mabadiliko ya kisera, kiteknolojia, na kiutendaji ambayo hujitokeza mara kwa mara katika mazingira ya kazi.

Mwalim Abdallah alitoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi kuhakikisha kuwa mafunzo yanakuwa sehemu ya mpango mkakati wa maendeleo ya rasilimali watu.

Aliongeza kuwa uwekezaji katika mafunzo ya watumishi si jambo la hiari  bali ni hitaji la msingi katika kufanikisha mageuzi na ufanisi katika utumishi wa umma na sekta binafsi kwa ujumla.

WASTAAFU watarajiwa kutoka katika wizara, idara na taasisi mbali za serikali wakipatiwa mafunzo elekezi kwa lengo la kujiandaa kukabiliana na maisha baada ya kustaafu.

USHIRIKIANO NA VYUO VYENGINE

Katika jitihada za kurahisisha utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa umma, Dk. Shaaban amesema IPA imeanzisha mashirikiano na  taasisi nyengine mbalimbai  ili kuhakikisha  mifumo ya utoaji wa mafunzo inaimarika na kukidhi mahitaji ya sasa ya kiutendaji.

Alieleza kuwa baadhi ya vyuo vya nchini Tanzania ambavyo tayari vimeshatiliana saini ushirikiano huo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Bara (TPSC) na kituo cha uhusinano wa kimataifa cha Dkt.Salim Ahmeid Salim (CFR).

Kwa upande wa  nje ya Tanzania, IPA imeingia makubaliano na Chuo cha Serikali ya Kenya (Kenya School of Government - KSG) uliojikita katika maeneo mbali mbali ya maendeleo ya kitaaluma na kiutawala.

Pamoja na hilo pia mafungamano hayo yatahusisha masuala ya kuandaa na kutekeleza programu za pamoja za mafunzo, kufanya tafiti za kisera na kiutendaji zinazolenga kurahisisha utoaji wa huduma serikalini pamoja na kubadilishana wataalam na wakufunzi kwa madhumuni ya kuongeza ubora wa mafunzo.

Aidha mkuu huyo, alibainisha kuwa chuo kitaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha  mitaala yake inaendana na mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya kiutawala yanayojitokeza kila mara.

UIMARA WA IPA

Kwa ujumla, IPA imekuwa nguzo muhimu ya mageuzi ya kiutumishi Zanzibar Kwa kutoa mafunzo yenye ubora wa hali ya juu, chuo hiki kinahakikisha kuwa watumishi wa umma wanakuwa chachu ya maendeleo, siyo kikwazo chake.

Kwa mfano katika mafunzo ya muda mfupi yanayotolewa na chuo hicho, yamekuwa kiungo muhimu cha kuhakikisha kuwa serikali inatoa huduma kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.

Kwa mantiki hiyo, IPA imekuwa injini ya mageuzi ya utumishi wa umma Zanzibar hivyo ni wajibu wa  taasisi ya serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kushirikiana na IPA katika kuimarisha uwezo wa watumishi wao kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Zanzibar.

Aidha kwa kuyafanya hayo, chuo hicho kitaendelea kuwa muhimili wa kuimarisha utendaji wa watumishi wa sekta ya umma kupitia mafunzo, tafiti  na ushauri elekezi.



Comments

Popular posts from this blog

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo