Takribani watu 50 hufariki kwa maradhi ya moyo duniani kila siku
NA MWANDISHI MAALUMU, ZANZIBAR
IMEELEZWA kuwa maradhi ya moyo na shinikizo la damu yanachangia takribani vifo vya watu milioni 20 kwa mwaka ulimwenguni, idadi ambayo ni sawa na vifo 50 kwa siku.
Akifungua mkutano wa tatu wa kimataifa wa maradhi ya moyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alieleza kuwa kwa Tanzania takribani watu milioni 4.9 wanasumbuliwa na magonjwa hayo ambayo huchangia asilimia 13 ya vifo vinavyotekea nchini.
Hivyo aliwahimiza washiriki wa mkutano huo kutumia fursa waliyoipata kujumuika pamoja kutafuta mbinu za kudhibiti ongezeko la magonjwa hayo kwa kujengeana uwezo na kuimarisha nyenzo za utendaji kazi ili kukabiliana na tabia zinazochochea magonjwa yasioyoambukiza hususani ya moyo na mishipa ya damu.
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, akielezea namna taasisi hiyo inavyofanya upasuaji wa kubadilisha valvu ya moyo bila kufungua kifua wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Aidha Hemed aliwataka washiriki hao kutumia mkutano huo kupata majibu sahihi katika maeneo muhimu yenye changamoto upande wa udhibiti wa magonjwa, ujuzi katika uchunguzi, matibabu na uendelevu wa huduma mpya zinazopatikana nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika taasisi hiyo pamoja na uimarishwaji wa sekta ya afya uliofanywa na Dk. Hussein Ali Mwinyi kupitia srerikali ya mapinduzi Zanzibar.
Aidha Dkt. Kisenge amesema JKCI ya sasa ni matokeo ya safari ya ubunifu iliyofanywa tangu mwaka 2015 ambapo sasa taasisi hiyo ina uwezo wa kufanya upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa 3,000 na upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 800 kwa mwaka.
AFISA Masoko wa kampuni ya Snibe Diagnostic, Vonnie Feng, akitoa maelezo juu ya huduma zinazotolewa na kampuni hiyo wakati walipotembelewa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
“JKCI ni miongoni mwa taasisi bora za matibabu ya moyo barani Afrika kwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, sasa tunaweza kufanya upasuaji wa kubadilisha valvu za moyo bila kufungua kifua ‘(Tavi Procedure)”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema mkutano huo unoshirikisha wataalamu wa maradhi ya moyo utawasaidia wadau wa sekta ya afya na kushirikiana kupata suluhisho litakalowasaidia wagonjwa wa moyo wanaowahitaji matibabu kutoka nchi mbali mbali duniani.
“Kupitia mkutano huu JKCI inaenda kuokoa Afrika katika masuala ya magonjwa ya moyo kwani sasa nchi za Afrika zinatutumia katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kama vile Malawi, Zambia, Comora na hivi karibuni Burkina Faso itatutumia”, aliongeza Dkt. Kisenge.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali Heart Team Africa Foundation (HTAF), Linda Gideon (kushoto), akimuonesha mmoja wa washiriki wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo bidhaa zinazouzwa na shirika hilo kwa ajili ya kukusanya fedha za matibabu ya watoto wenye maradhi ya moyo wanaotibwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Comments
Post a Comment