ZBS kuifanya Z'bar kitivo cha maabara Afrika

NA MWANDISHI MAALUM, ZANZIBAR

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Yussuph Majid Nassor, amesema kuwa taasissi hiyo inatarajia kujenga maabara kubwa katika eneo la uwekezaji wa viwanda liliopo Dunga Zuzeitakayokuwa kitivo cha maabara Afrika.

MKUU wa usalama wa bandari ya Fumba, Juma Ali (kulia) akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo kukagua kazi za taasisi ya viwango Zanzibar (ZBS) ikiwa ni sehemu ya Jukwaa la Viwango 2025 lililoandaliwa na ZBS. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya ZBS, Balozi Omar Yussuf Mzee, ktikati ni mkurugenzi mkuu wa ZBS, Yussuf majid Nassor. 

Majid alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake Maruhubi baada ya waandishi na watendaji wa taasisi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Balozi Omar Yussuf Mzee, kutembelea maabara mbali mbali za taasisi hiyo na bandari za fumba na bandari kavu ya maruhubi kuangalia namna taasisi hiyo inavyofanya kazi.

Ziara na mazungumzo hayo ni sehemu ya Jukwaa la Viwango linaloandaliwa na taasisi hiyo kila mwaka na kuratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) ambapo Majid alieleza kuwa ujenzi wa maabara hizo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36 kutoka sasa.

MENEJA wa bandari kavu (ZMT) ya Maruhubi, Evans Samwel Ruta, akiwapatia maelezo kuhusu shughuli za bandari hiyo waandishi wa habari na watendaji wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) waliotembelea bandari hiyo ikiwa ni sehemu ya Jukwaa la Viwango 2025 lililoandaliwa na taasisi hiyo. Wa pili kushoto niulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya ZBS, Balozi Omar Yussuf Mzee. 

Alifafanua kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutaitangaza Zanzibar na kuwa kitivo cha maabara katika ukanda wa Afrika mashariki na kati hivyo kukuza na kuimarisha biashara kati ya Zanzibar na maeneo mengine ulimwenguni.

Alisema tasnia ya ujenzi Zanzibar imekuwa kubwa na ndio maana wanajenga maabara nyingi na tayari wamejenga maabara kubwa ya vifaa vya ujenzi ili vifaa hivyo vipimwe Zanzibar.

Alisema awali wawekezaji walikuwa wakipeleka vifaa vyao vya ujenzi Tanzania bara kwa ajili ya kupima ubora.

AFISA Uhandisi ujenzi wa maabara ya ujenzi za ZBS, Salim Kassim Juma (kushoto), akitoa maelezo waandishi wa habari kuhusu ufanyaji kazi wa maabara hizo wakati wa ziara ya waandishi wa habari.

Alisema ZBS ilianza na maabara nne lakini kwa sasa inamaabara 10 na ndani ya miezi minne ijayo itakua na maabara 13 ili kukidhi kiu ya uingiaji wa mizigo Zanzibar na kumlinda mtumiaji wa mwisho.

Alisema bado kuna changamoto ya upimaji ubora wa vifaa kisiwani Pemba ambapo vifaa hutoka Pemba na kupimwa Unguja hivyo pia serikali inatarajia kujenga maabara kisiwani humo.

Alisema serikali imejikita katika maabara ya uchumi ya buluu ambapo, watapima viwango vya ubora wa uvuvi ikiwemo samaki, dagaa, mwani, gesi na mafuta.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ZBS, Balozi Omar Yussuf Mzee, alisema kazi ya kuelimisha taifa sio kazi ndogo hivyo aliwapongeza waandishi wa habari kwa kazi kubwa wanayoifanya.


Alisema waandishi wa habari wana umuhimu mkubwa kwa ZBS kwasababu lengo la uwepo wa taasisi ni kumlinda mlaji kwa kuhakikisha bidhaa zinazoingiza zinakuwa na ubora.

 "Tunawahitaji sana waandishi wa habari maana ndio mtakaotusaidia kutoa elimu, sisi hatuna midomo ya kuwafikia watu wote lakini nyinyi mna uwezo huo wa kutoa elimu kwa umma", alisema.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo