ZEC yataka mijadala ya uchaguzi ihusishe wataalamu wa uchaguzi
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
MKURUGENZI wa uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, amesema kuwa kuitisha mijadala inayohusiana na uchaguzi kwenye vyombo vya habari bila ya kuwepo wataalamu wa tume ni kosa kisheria.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki visiwani hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) katika mkutano mkuu na mafunzo yaliyodhaminiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Mashirika yay Umma (PSSSF).
Alisema kuna baadhi ya vyombo vya habari vinaendesha mijadala kwa kuhusisha watu wasiokua na majibu sahihi kuhusu uchaguzi na kuwaweka njia panda jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Aidha alivitaka vyombo vya habari vinavyotaka kuendesha mijadala kuhusu uchaguzi ni vyema kuwasiliana na Tume ya Uchaguzi ili vipatiwe maafisa watakaotoa majibu sahihi kwa masuala yatakayoulizwa.
"Hii ni rai kwenu nyinyi waandishi wa habari ni busara zaidi kama kuna mijadala inaendeshwa katika vyombo vya habari ni vyema mkatualika na hatutosita kuleta afisa wetu kutoa ufafanuzi kuhusu masuala yanayohusu uchaguzi", alisema Faina.Alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi namba nne ya mwaka 2018 inaeleza kuwa kutoa taarifa za uchaguzi bila ya ruhusa ya tume ni miongoni mwa makosa.
"Mtu atakayefanya kosa hilo akitiwa hatiani atalipa faini isiyopunguwa shilingi 200,000 na isiyozidi shilingi 5,000,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela na kisichozidi mwaka mmoja au adhabu zote mbili kwa maana ya faini na kifungo", alifafanua Mkurugenzi hiyo na kuwashauri wanahabari kuepuka kutenda makosa hayo badala yake kufanyakazi kwa weledi na kuacha ushabiki.
Aidha Faina alipongeza PSSSF kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na ZPC kutoa mafunzo kwa waandishi kwa sababu ni kioo cha jamii.
Naye Meneja wa PSSSF ofisi ya Zanzibar, Rajab Shabani Kinande, alisema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuelimisha umma kuhusu mambo mbali mbali katika nchi hivyo mafunzo hayo yawe chachu ya kujenga mustakabali mwema wa jamii na taifa' kwa ujumla.
Aliongeza kuwa mfuko huo kama moja ya mifuko ya hifadhi ya jamii inategemea vyombo vya habari kuwafikia wanachama wake na jamii hivyo aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wanahabari kupitia ZPC ili kuifikia jamii kwa haraka lakini pia kupata mrejesho kuhusiana na huduma wanazozitoa.
Naye Mwenyekiti wa ZPC, Abdallah Mfaume, aliwasisitiza waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa karibu na ZEC lakini pia PSSSF kwa lengo la kurahisisha utoaji wa habari sahihi kwa umma.
Comments
Post a Comment