2.4trl/- kuing'arisha elimu 2025/26
NA SAIDA ISSA, DODOMA
WAZIRI ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeomba kuidhinishiwa shilingi trilioni 2.4 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika kipindi hicho, Serikali
itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa elimu na umma kuhusu sera ya elimu na
mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023 pamoja na utekelezaji wa mitaala
iliyoboreshwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara
hiyo, alisema Serikali imepanga kutoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule,
walimu wa shule za msingi na sekondari, wakufunzi wa vyuo vya ualimu, maafisa
elimu, wakufunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja
na wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu.
Alieleza kuwa serikali itakamilisha
mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ili iendane na matakwa ya Sera ya Elimu
na Mafunzo 2014 (Toleo la 2023), sambamba na mapitio ya sheria nyingine za
taasisi mbalimbali zinazohusika na elimu kama vile Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH), Bodi ya Huduma za Maktaba, Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA), Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), na taasisi
nyingine zinazotoa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Aidha Prof. Mkenda alisema
Serikali itakamilisha zana muhimu za utekelezaji wa sera, ikiwemo Mwongozo wa
Upimaji na Tathmini katika Elimu, Mfumo wa Taifa wa Upimaji na Tathmini, na
Mfumo wa Taifa wa Mitaala ili kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa sera
hizo.
“Serikali itaandaa na kuhuisha
miongozo mbalimbali inayohusu utoaji wa elimu na mafunzo, ikiwa ni pamoja na
mwongozo wa kiunzi cha mahitaji ya walimu na usambazaji wao kwa lengo la
kuimarisha usawa kulingana na mahitaji ya shule”, alieleza Prof. Mkenda.
Kadhalika alisema kuwa serikali pia
itaandaa mwongozo wa kitaifa wa kuwaendeleza kitaalamu wakufunzi na wafanyakazi
wasio wakufunzi katika vyuo vya elimu ya ufundi.
"Mwongozo wa ushirikiano
baina ya viwanda na taasisi za elimu ya ufundi, Mwongozo wa Utambuzi wa Ujuzi
katika Elimu ya Ufundi, Mwongozo wa kushughulikia masuala mtambuka katika
taasisi 49 za elimu ya juu, Vilevile serikali itaandaa mwongozo wa uanzishaji
wa kampuni na vituo vya ubunifu wa teknolojia (TICs) katika taasisi za elimu ya
juu (umma na binafsi) na taasisi za utafiti wa maendeleo (RDIs), pamoja na
kuhuisha miongozo ya udahili, upimaji, ithibati, elimu ya watu wazima, na elimu
nje ya mfumo rasmi", alisema.
Kwa mara ya kwanza, Serikali
itaanzisha programu ya Mama Samia 360 – DSP/AI+, itakayotoa ufadhili kwa
wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu katika masomo ya sayansi (kidato cha
sita) kusomea shahada ya kwanza kwenye vyuo vikuu mahiri duniani katika fani za
Data Science, Artificial Intelligence (AI), na Machine Learning (ML).
Katika eneo la sayansi na
teknolojia ya nyuklia, Serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wenye
ufaulu wa juu kwa ngazi ya shahada na shahada ya juu kupitia SAMIA Extended
Scholarship.
Pia serikali itaanza utekelezaji
wa SAMIA Innovation Fund yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya
kutoa mikopo nafuu kwa wabunifu, ili kuwezesha ubunifu kubiasharishwa na kutoa
ajira kwa Watanzania.
"Ili kuchochea tafiti bora,
Serikali itaendelea kutoa tuzo ya Shilingi milioni 50 kwa tafiti zitakazochapishwa
katika majarida ya kimataifa yenye hadhi ya juu, serikali itaendeleza elimu ya
amali kwa kupanua shule 55 kuwa sekondari za amali, kuimarisha miundombinu ya
vyuo vya ualimu wa amali (Mtwara Kawaida na Ufundi), na kuanzisha vyuo vipya
vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi", alisema.
Serikali pia itajenga na
kukarabati vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi, kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa
Chuo cha Ufundi Dodoma (ikiwa ni pamoja na mabweni, maktaba, karakana, nyumba
za watumishi, na ukuta), na maktaba ya kisasa katika Chuo cha Ufundi Arusha.
Mradi mwingine utahusisha ujenzi
wa mtambo wa nguvu za maji Kikuletwa na kupanua maabara ya udongo Arusha.
Vilevile, Serikali itatekeleza Mradi wa TELMS II kwa ajili ya kuanzisha vituo
vya ujasiriamali na ubunifu katika taasisi mbalimbali.
Serikali itaongeza idadi ya
wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 245,314 mwaka 2024/25 hadi
252,773 mwaka 2025/26. Vilevile, mikopo kwa wanafunzi 10,000 wa stashahada
katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati itaendelea kutolewa.
"Ufadhili kupitia SAMIA
Scholarship utatolewa kwa wanafunzi 2,630 wenye ufaulu wa juu, ikiwa ni pamoja
na wanafunzi 50 wa kike waliomaliza kidato cha sita,
Serikali pia itaendelea kuboresha
ukusanyaji wa mikopo iliyoiva yenye thamani ya Shilingi bilioni 210.2 na
kutambua wanufaika wapya 40,000,"alisema.
Prof. Mkenda alisema Serikali
itakamilisha mapitio ya muundo wa COSTECH, kuboresha mifumo ya TEHAMA
inayounganisha taasisi za elimu na utafiti, kufadhili tafiti 40 (19 kuhusu
tabianchi na 21 viwanda), na kuendelea kugharamia vigoda vya utafiti katika
taasisi za Nelson Mandela na SUA.
Serikali itaendelea kuandaa Dira
ya Taifa ya Teknolojia 2050 itakayohusisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu,
lugha, biashara, afya, kilimo, haki za binadamu na TEHAMA kwa maendeleo
endelevu ya Taifa.
Comments
Post a Comment