Mbunge Ikupa ahimiza wenye ulemavu kulinda amani
NA SAIDA ISSA, DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalum Stella Ikupa amewahimiza watu wenye ulemavu kuendelea kuenzi hali ya amani na utulivu vilivyopo nchini na kuwataka kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza wakati akifungua
kongamano la watu wenye ulemavu lililoandaliwa na Ikupa Trust Fund alisema watu
wenye ulemavu ni moja ya makundi ya Mwanzo yatakayopata shida kama machafuko
yatatokea kwa sababu yoyote ile .
"Ninawaomba ndugu
zangu,tunapoelekea katika uchaguzi mkuu, tuendelee kuiombea nchi yetu amani
iendelee kudumu, tusikubali kuwa sehemu ya jambo lolote ambalo ni kinyume ,maana
machafuko yakitokea nchini ,sisi walemavu ndio waathirka wa kwanza, tukifiatiwa
na akina mama na watoto, tumuombe Mwenyezi Mungu uchaguzi uwe wa amani, tukatae
wanahamasisha virugu”, alisema Ikupa.
Aidha Ikupa alitumia fursa hiyo
kuipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mambo
mengi iliyifanya kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
"Serikali ya awamu ya sita
imeendelea kufanya mambo makubwa kwa watanzania lakini yapo mambo maalum
yanayowagusa watu wenye ulemavu ikiwemo ujenzi wa miundombinu katika majengo ya
Serikali na yasiyo ya serikali kwa ajili ya watu wenye ulemavu”, alisema Mbunge huyo.
Katika hatua nyingine ameishukuru
serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuweka utaratibu wa kuwapata
wawakilishi wa watu wenye ulemavu Bungeni lakini pia kumpa fursa na kuhudumu
kama Mbunge katika kipindi chake chote cha uongozi.
Kadhalika aliviomba vyama vyote kuweka
utaratibu wa kuwapata wawakilishi wao watakaoingia Bungeni kupitia kundi la
wenye ulemavu Ili kuongeza wigo wa watunga sera kupitia kundi hilo.
"Lakini na sisi tuzungumze
huko kwenye vyama vyetu kwamba tunahitaji nafasi hizo tusikae kimya tukitegemea
kuna mtu mwingine atatuzungumzia kile tunachohitaji”, alisema.
Hivyo aliwataka washiriki wa kongamano
hilo, kwenda kuelimisha na wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria
kongamano hilo huku akihimiza viongozi wa vyama vya wenye ulemavu waendelee
kuongeza wanachama Ili iwe rahisi kupata huduma maeneo mbalimbali ikiwemo serikalini.
Comments
Post a Comment