Msiwanyanyapae watoto wenye ulemavu – DC Hamid
MKUU wa wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said (pichani), amewataka wazazi kutowaficha na kuwanyanyapaa watoto wenye ulemavu badala yake wawajumuishe kwenye shughuli mbali mbali ili wapatiwe haki zao na kushiriki katika maendeleo.
Amesema watoto wenye ulemavu wana
haki sawa na watoto wengine hivyo kuna ulazima wa jamii kutambua umuhimu wa
kundi hilo kuunnga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali kuwapatia haki zao.
“Serikali imechukua hatua mbali
mbali ikiwa ni pamoja na kujenga skuli maalum za watoto wenye ulemavu zenye
miundombinu inayokidhi mahitaji yao pamoja na kuajiri walimu wenye ujuzi wa
kufundisha watoto wenye ulemavu”, alieleza DC Hamid.
Sambamba na hilo ameeleza kuwa serikali
pia imeimarisha huduma za afya katika hospitali zake hususani kitengo cha
marekebisho na mazoezi ya viungo ili kuhakikisha watoto hao wanapatiwa huduma zinazostahiki
za kupunguza athari za ulemavu wao.
MKUU wa Wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said (katikati), akimlisha keki mmoja ya watoto wenye ulemavu baada ya kuzindua Tamasha la Furaha Jumuishi kwa Watoto wenye Ulemavu lililoandaliwa na ofisi hiyo.
Aidha amesisitiza kuwa ni vyema watoto hao wakashirikishwa katika sekta zote, ikiwemo michezo ili kuhakikisha wanapata haki na fursa sawa kama watoto wengine huku akikemea tabia ya baadhi ya wazazi wa kiume ya kuwatelekeza watoto wenye ulemavu.“Aidha natumia fursa hii kuwataka kina baba wenzangu wenye tabia ya kutlekeza familia zao au watoto wao wenye ulemavu kuacha kufanya hivyo badala yake washirikiane na familia zao katika malezi na matunzo ya watoto hao ili kuwasaidia watoto kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo”, alisema Mkuu huyo wa wilaya.
MKUU wa Wilaya ya Mjini, Hamid Seif Said (katikati), Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe na Mwalimu wa elimu maalum, Happy Johnson (wa pili kulia), wakiwa katika picha na watoto wenye ulemavu wa mtindio wa ubongo wakati wa Tamasha la Furaha Jumuishi kwa Watoto wenye Ulemavu wa wilaya ya Mjini.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe, amesema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, inaonesha kuwepo kwa ongezeko la watu wenye ulemavu waliofikia asilimia 11.4 ya watu wote kutoka asilimia 5.8 waliopatikana katika sensa ya mwaka 2012.
“Idadi hiyo inaonesha kundi hilo
limeongezeka hivyo mikakati madhubuti inahitajika kuhakikisha tunadhibiti
lisiongezeke lakini kwa waliopo wanapatiwa haki zao na huduma stahiki ili
waweze kupiga hatua kubwa za maendeleo”, amefafanua Mhandisi Debe.
Mwenyekiti
wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Salma Saadati Haji, akimpongeza mmoja ya watoto wenye
ulemavu walioshiriki Tamasha la Furaha Jumuishi kwa Watoto wenye Ulemavu wa
wilaya ya Mjini.
"Harakati za kupigania haki za watu wenye ulemavu zilianza miaka mingi, tunashukuru kuona sasa hatua mbali mbali zinachukuliwa ili kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu wanapata haki na stahiki zote kama iivyo kwa watu wasio na ulemavu", amesema Mwenyekiti huyo.
Katika hafla hiyo, watoto wenye aina mbali mbali za ulemavu walishiriki michezo na matukio mbali mbali huku wazazi wa watoto hao wakitoa ushuhuda wa mafanikio waliyoyapata na changamoto wanazopitia kuwalea na kuwatunza watoto wao.
Comments
Post a Comment