Naibu Waziri azindua miradi ya kiuchumi ya watu wenye ulemavu
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga amezindua miradi ya kiuchumi ya shirika la Strategic Alternative Learning Technique (SALT), inayohudumia vijana wenye changamoto za ufahamu.
Nderiananga alifanya uzinduzi huo jijini Dar es Salaam kwa miradi ambayo ni pamoja na SALT Special Supermarket,
Mgahawa na Bekari itakayohudumiwa na vijana wenye ulemavu wa ufahamu huku
akisema jumla ya vijana na Watoto 83 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutoa
huduma kwa wananchi hatua itakayowasaidia kujipatia kipato chao na kuchangia
maendeleo ya Taifa.
Aidha aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ikiwemo elimu, kujiwezesha kiuchumi na kusaidia mashirika yanayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.
“Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa fedha kwa watu wenye ulemavu ili wafanye kazi zao vizuri. Nimefurahi kuona Shirika hili la SALT linafanya kazi zake kwa ubunifu kwa kuwafundisha stadi za kazi na ubunifu wa mavazi,” alisema Nderiananga.
Vilevile, alifafanua kwamba ikiwa kila mmoja atafanya kwa nafasi yake katika kuwawezesha watu wenye ulemavu itaongeza chachu kwao kujituma kufanya kazi kwani vipaji na uwezo wao utatambulika na kuungwa mkono hali itakayoongeza uzalishaji katika Nchi.
“Nitoe wito tuendelee kuliunga mkono Shirika hili na mengine yanayowasaidia watu wenye ulemavu wa aina zote kwani yanafanya kazi kubwa hivyo viongozi wetu wa Serikali za Mitaa tuyapokee mashirika haya na kuwapa ushirikiano kwa manufaa ya Taifa letu”, alieleza Naibu Waziri huyo .
Aidha alibainisha kwamba watu wenye ulemavu wanahitaji fursa bila kunyanyapaliwa huku akiwataka wazazi na walezi kutosikiliza maneno ya kukatisha tamaa na badala yake wawaamini watoto wao kuwa wana uwezo wa kipekee.
Aliwahimiza wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu kutumia fursa za mafunzo yanayotolewa katika taasisi mbalimbali ili kuwajengea Watoto kujiamini kuwa wanaweza na wanamchango katika jamii.
Alizitaja baadhi ya bidhaa hizo kuwa ni sabuni za kuogea, shampoo, mafuta ya kupaka, vitambaa vya batiki, mikate na ufugaji wa samaki, kuku pamoja na bustani za mboga mboga.
“Kituo hiki kilianzishwa kwa lengo la kuwawezesha vijana wenye changamoto za kiakili na ufahamu kupata stadi za kazi, stadi za maisha na mazingira salama ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kiuchumi. Lengo letu kuu ni kuwapatia fursa ya kujitegemea, kuongeza thamani katika maisha yao na kupunguza utegemezi kwa familia au jamii”, alieleza Meneja huyo.
Comments
Post a Comment