NBC yaahidi kumuunga mkono Rais Samia kuimarisha ustawi wa wafanyakazi
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kubuni huduma mahususi za kibenki kwa ajili ya makundi mbali mbali ya watumishi wa umma na sekta binafsi ili kuchochea kasi ya ukuaji uchumi kupitia rasilimali watu.
Hatua hiyo pia ni kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa tanzania inayoongozwa na rais, dk. Samia Suluhu hassan inayolenga kuimarisha maisha ya wafanyakazi na kukuza ujumuishaji wa kifedha.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa benki hiyo, Godwin Semunyu, alieleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari kupongeza hatua ya serikali kupitia Rais Dk. Samia kutangaza ya nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 370,000 hadi shilingi 500,000 sawa na ongezeko la asilimia 35.1.
Dk. Samia alitangaza uamuzi huo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Bombadia, mkoani Singida hivi karibuni ambapo benki hiyo ilikuwa miongoni mwa wadhamini wa maadhimisho hayo yaliyoratibiwa na Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
“Mbali na sisi wenyewe kuwa ni sehemu ya wafanyakazi wa umma, ushirikiano wetu na wafanyakazi wengine unaimarishwa zaidi kupitia huduma tunazozitoa kwao kwa kuzingatia mahitaji yao mahususi ikiwemo kuwatunzia amana zao kupitia akaunti mbali mbali kulingana na machaguo yao”, alieleza Semunyu.
Kwa mujibu wa Semunyu, kufanya hivyo pia kunawarahishia huduma za miamala pamoja utoaji wa huduma za mikopo ya aina mbali mbali iliyobuniwa mahususi kwa ajili ya wafanyakazi.
Alieleza kuwa ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia, benki hiyo itaendelea kutoa mikopo ya muda mrefu na muda mfupi yenye masharti rafiki kwa wafanyakazi ili kuboresha maisha yao kupitia uwezeshaji utakaongeza kasi ya wao kumiliki nyumba za kisasa, kununua vyombo vya usafiri na vitendea kazi mbalimbali ili kufanikisha majukumu yao.
Comments
Post a Comment