Dk. Samia aitaka mahakama kusimamia haki

NA MWANDISHI WETU 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema matarajio ya Watanzania ni kuona mahakama inasimamia haki.

Kauli hiyo alitoa Juni 15, 2025 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, wakati akimuapisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Mcheche Masaju, aliyemteua hivi karibuni.

Aidha alisema Watanzania wanatarajia kuona mahakama inaendelea zaidi kutoka ilipo sasa kuanzia majengo, vitendea kazi na mifumo.

Aidha alirejea kauli yake aliyoitoa katika kilele cha siku ya sheria mwezi Februarimwaka huu, kwamba  kazi ya Majaji ni kusimamia haki na  kazi ya kutoa haki  ni ya Mwenyezi Mungu.

“Sisi Majaji hatuna kudra wala jaala, kazi yetu ni kusimamia haki kwa misingi tuliyojiwekea, hivyo msisitizo wangu twendeni tukasimamie haki”amesisitiza Dk. Samia.

Amesema serikali kwa upande wake itafanya kila linalowezekana kuendelea kufanyia kazi changamoto za mahakama kama alivyoahidi wakati akihutubia bunge kwa mara ya kwanza Aprili 22, 2021.

Aidha, alimuomba Jaji Masaju kuendelea kuyafanyia kazi mapendelezo ya Tume ya Haki Jinai kwa kuainisha yaliyotekelezwa na mambo ambayo bado hayajatekelezwa ili serikali ione namna ya kuyatekeleza.

Vile vile amempongeza Jaji Mkuu mstaafuProf. Ibrahim Hamis Juma, kwa kumaliza muda wale wa utumishi, akisema wakati anazungumza hajawahi kumuona akiwa na furaha kama aliyonayo sasa.

“Amefanya kazi kubwa ya kuleta mageuzi ndani ya mahakama, kuleta mageuzi ya kimiundombinu pamoja na kushirikiana na serikali na bado ameacha kazi inaendelea, ambapo katika mifumo amefanya kazi nzuri Dodoma kwa kuwepo chumba ambacho unaona kesi zinavyoakhirishwa, zinavyoendelea na kutolewa hukumu, hivyo umeacha alama kubwa katika mahakama”, alisema Dk. Samia.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo tathmini ya kidunia inaonesha jinsi imani  ya wananchi kwa mahakama inavyopanda.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alimpongeza Rais Samia kwa kutekeleza majukumu yake vizuri na kwa mafanikio.


Pia alimpongeza Jaji Masaju kwa kuwa mtumishi bora katika sekta ya mahakama na kumuahidi ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake Jaji Mkuu Masaju, alimshukuru Rais Samia kwa kumuona anafaa kuongoza muhimili huo ambapo kazi yake ni kutoa haki kwa watu wote bila ya kujali hali ya mtu kuichumi na kijamii.

Mapema Jaji mstaafu, Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisema lazima jicho la Jaji Mkuu likamate jicho la Rais, amuangalie anachofanya na kusaidia mahakama katika kutekeleza miradi. 

Aidha alimshukuru Rais Samia kwa kumuamini pamoja na aliyekuwa Rais Hayati, Dk. John Pombe Magufuli kwa nafasi hiyo huku akimsisitiza Jaji Masaju kumaliza miradi inayoendelea kutekelezwa katika maneno mbali mbali nchini.

Alisema Rais Samia amewezesha upatikanaji wa dola milioni 65 kutoka Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kuimarisha mahakama kwa sababu anajua utaoji wa haki ni sehemu ya maendeleo ya nchi.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

'Zanzibar Matibabu Card' yashinda tuzo ya WSIS

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

ZAMECO yakumbushia sheria mpya ya habari