Dk. Samia asema daraja JP Magufuli litafungua fursa usafirishaji kikanda

NA MWANDISHI WETU, MWANZA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua daraja la JP Magufuli maarufu kama Kigongo - Busisi, mkoani Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo Juni 19, 2025 Rais Samia, alisema daraja hilo linafungua historia mpya katika sekta ya usafiri na usafirishaji kati ya Kigongo na Busisi.

Akizungumza na wananchi, alisema aliendeleza ujenzi wa mradi huo uliosisiwa na Rais John Pombe Magufuli kutokana na ahadi yake kwa Watanzania ni kuyaendeleza mambo yote yaliyoachwa na viongozi wa awamu zilizopita na pia kutekeleza mengine mapya.

“Leo tunaandika historia mpya kuhakikisha hadithi za kusikitisha zinaondoka juu ya usafisi na usafirishaji”, alisema.

Alisema alipokea mradi huo ukiwa umefikia asilimia 25 kwa gharama ya shilingi bilioni 152 ambazo zililipwa kwa wakandarasi, lakini serikali yake imefanikiwa kuendeleza ujenzi wa daraja hilo lenye umuhimu mkubwa kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Alifafanua kuwa daraja hilo limejengwa kwa lengo la kuunganisha barabara za Usagara na Sengerema katika Ziwa Victoria, ambayo ni mihimu katika ushoroba wa kiuchumi katika kanda hiyo.

Alisema sasa wananchi watatumia takribani dakika nne kuvuka kufika Busisi kwa kutumia gari na wanaotembea kwa miguu watatumia muda mfupi.


Alisema ujenzi wa daraja hilo uliogharimu shilingi bilioni 718 umetekelezwa kwa fedha za ndani zinazotokana na kodi, akiongeza kuwa litakuwa alama na uthibitisho kwamba serikali imepiga hatua ya kuifanya Tanzania kuwa taifa kubwa kiuchumi na ishara ya kupanga, kutekeleza na kufanikisha mipango mikubwa.

Aidha, alisema asilimia 92 ya wafanyakazi katika mradi huo walikuwa Watanzania  huku akiongeza kwamba daraja hilo linatokana na wazo la Watanzania wenyewe.

Alisema daraja hilo ni la kimkakati na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kujipanga kulilinda.

Awali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alimpongeza Rais Samia, akisema ana mapenzi mema na Watanzania, akisema miradi yote waliyoianzisha pamoja na Rais hayati, Dk. Magufuli, imetekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Naye Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alimshukuru Rais Samia kwa maelekezo yake kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika na kuongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne amewalipa wakandarasi zaidi ya shilingi bilioni 450 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Alisema yale yote aliyowaahidi Watanzania wakati akilihutubia bunge kwa mara ya kwanza mwaka 2021, ameyatekeleza kwa mafanikio, akisema daraja hilo ni kielelezo kwa Tanzania cha kufanya maamuzi kwa maendeleo yake akiongeza kuwa kanda ya Ziwa imewekewa msisitizo mkubwa kiuchumi ambao utazalisha fursa nyingi za ajira.


Daraja hilo ni la sita kwa urefu Afrika, limejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 718, ambapo ujenzi wake umefanywa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway 15 Bureau Group Corporation.

Kwa mujibu wa taarifa, daraja hilo lenye urefu wa kilomita tatu, upana wa mita 28.45 za barabara za kuunganisha zenye urefu wa kilomita 1.66 lilianza kujengwa Februari 2020, pia lina njia mbili za gari zenye upata wa mita saba kila upande na njia za watembea kwa miguu kila upande zenye upana wa mita 2.5 na maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande likipita juu ya maji ya Ziwa Victoria kuunganisha eneo la Kigongo liliopo wilaya ya Misungwi na Busisi wilaya ya Sengerema.

 

Comments

Popular posts from this blog

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo