NBC yaahidi makubwa ligi kuu Tanzania bara
NA MWANDISHI WETU
MDHAMINI Mkuu wa ligi ya NBC, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC)
jana ilikabidhi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya soka ya NBC (NBCPL) kwa timu ya
Yanga SC ya jijini Dar es Salaam iliyoibuka bingwa wa kombe hilo msimu wa
mwaka 2024/2025.
Hafla ya kukabidhi ubingwa huo
ilifanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dare es Salaam baada ya mchezo
wa mwisho wa ligi hiyo baina ya mabingwa hao na Simba SC ya jijini uliomalizika
kwa yanga kuibuka na ushindi wa magoli 2 - 0.
Hafla hiyo iliongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Shirikisho la
Mpira wa Miguu nchini (TFF), Athuman Nyamlani na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald
Sabi, ambao kwa pamoja walikabidhi kombe hilo.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Sabi
pamoja na kuwapongeza mabingwa hao na timu nyngine zilivyoshiriki ligi hiyo,
alieleza kutiwa zaidi na kasi ya maendeleo a mchezo wa soka nchini hususani
ushindani mkubwa unaoshuhudiwa kila msimu.
“Tangu tuanze kudhamini, tumeshuhudia ushindani mkubwa na wa
kuvutia kati ya vilabu vyote vinavyoshiriki. Ushindani huu siyo tu umepandisha
kiwango cha mchezo, bali pia umetufanya tushuhudie matukio ya kusisimua na
burudani ya hali ya juu”, alieleza Sabi.
Aliongeza kuwa hali hiyo
inadhihirisha kwamba kila timu inajitahidi kuonesha uwezo wake wa hali ya juu,
na hili ni jambo la kufurahisha sana kwetu kama wadhamini.
“Tunapofunga mwaka huu wa mashindano, tunatambua kwamba
ushindani ni sehemu muhimu ya maendeleo ya michezo na tunajivunia kuwa sehemu
ya safari hii. Napenda kuwahakikishia wapenzi wa mchezo huu kuwa Benki ya NBC
itaendelea kuboresha udhamini wa Ligi Kuu ya NBC msimu ujao”, alisema Sabi.
Sabi alitaja jitihada zinazohitaji
kipaumbele kuwa ni pamoja na uwezeshaji kwenye michakato ya mafunzo na
maendeleo ya wachezaji hususani kwenye programu za vijana, huduma bora za bima husasani
ya afya kwa wachezaji na huduma za kibenki mahususi kwa wanamichezo.
Comments
Post a Comment