Viwango bora nyenzo muhimu kukuza masoko kimataifa - Dk. Mwinyi
NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa usimamizi bora wa viwango vya bidhaa ni nyenzo muhimu kwenye biashara na kukuza masoko kimataifa.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla (pichani), alipokuwa akifungua mkutano wa 31 wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), uliofanyika hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege , Zanzibar.
Alieleza kuwa serikali za Tanzania zinaelewa jukumu kuu la viwango katika kuwezesha matumizi ya viwango katika biashara kati ya nchi za Afrika, kukuza usalama wa watumiaji na kuimarisha ushindani wa viwanda.
Aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kuendelezwa kwa mikusanyiko na majukwaa kama mkutano huo kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya kusimamia miongozo ya viwango Afrika na kuipongeza ARSO kwa kuendelea kujitolea kuendeleza ubora na kuunganisha miundombinu kila pahala Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Biashara na maendeleo ya viwanda, Omar Said Shaaban, wakiziindua kitabu cha muongozo wa kuhamasisha viwango vya uwekezaji na biashara Afrika.
Aliongeza kuwa mtazamo huo unalingana na uzoefu wa kimataifa hasa kanuni ya ‘Hati ya ‘Kiwango Kimoja- Kipimo Kimoja – Inayokubaliwa Kila pahala’ hivyo aliiomba ARSO kuendelea kufanya kazi pamoja kwa kuunganisha mifumo ya uthibiti ya Afrika kwa ufanisi na kusaida ushindani wa bara l la Afrika.
“Umuhimu pia utolewe kurahisisha mifumo ya udhibiti ya Afrika juu ya kuwa na viwango, vyeti na kanuni sawa chini ya taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Umoja wa Taasisi za Viwango Afrika (ARSO) na Miundombinu ya Ubora wa Pan-Afrika (PAQI)”, alieleza Dk. Mwinyi.
Alisema katika kuhakikisha hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha ZBS ili itekeleze majukumu kwa ufanisi ili kustawishaji wa biashara, kuongeza ushindani na upatikanaji wa masoko kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alieleza kuwa suala la viwango vya ubora sio la hiari ni suala bali ni la lazima hasa katika maendeleo ya biashara na ukuaji wa uchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma za Afrika.
Alisema hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa uwezo wa ushindani kimataifa pamoja na kulinda maslahi ya watumiaji hivyo Zanzibar itaendeleza mpango wa kuwa maabara zenye vifaa vya kisasa zitakazoidhinisha viwango vya bidhaa zinazozalishwa au kuingia nchini.
Mbali ya kuimarisha maabara, pia serikali itaendelea kuwekeza kwenye rasilimali waku kwa kuwapatia ujuzi na maarifa watendaji wa taasisi za viwango, kuimarisha sera, taratibu na Jumuiya ya Biashara katika kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa viwango.
“ARSO inatupatia jukwaa la ushirikiano wa kiutendaji kati ya nchi za Afrika na watoa viwango bingwa wa kimataifa. Hii inalenga mpango thabiti wa kubadilishana uzoefu, teknolojia na kufungua soko zaidi”, alieleza Waziri Shaaban na kupongeza uamuzi wa jumuiya hiyo kufanyia mkutano huo Zanzibar.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla (katikati), akiwa na viongozi wa kitaifa, ISO na ARSO wakipokea nyimbo za taifa.
Alifahamisjha kuwa kupitia mkutano huo viwango mbali mbali vitathibitishwa kupitia kamati za kitaalamu na kushihisha baadhi yao ili kuwa na mlingano miongoni mwa nchi wanachama hivyo kurahisisha biashara miongoni mwao.“Kuwepo kwetu hapa kunaweka mkazo katika uimarishaji wa viwango lakini pia ushindani kwenye uzalishaji hivyo kuhimiza kuwa na mageuzi ya sera, mifumo ya kibiashara, kujenga uwezo na kuweka mifumo ya ubora ya udhibiti na kukuza utamaduni wa ubora wa viwango ambao ni muhimu katika uchumi wa soko huria”, alieleza Dk. Nsengimana.
Awali Mkurugenzi wa TBS, Dk. Ashura Kantunzi, alisema mkutano huo unatoa nafasi ya kutafakari kwa kina juu ya namna bora ya kuandaa mazingira ya biashara kwa kuzingatia uwazi, heshima na kuhakikisha usawa kwa wazalishaji wa Afrika hasa wafayabiashara ndogo ndogo na za kati.
“Taasisi zinazosimamia viwango nchini, ZBS na ZBS zina mpango wa kusaidia biashara ndogo na za kati kwa kutambua kuwa ndio injini ya uchumi wa nchi kwa kuwapa miongozo iliyorahisishwa ya viwango na mafunzo yaliyolenga kukidhi mahitaji ya ubora wa biashara chini ya AFCFTA na kuhakikisha faida ya biashara huria”, alieleza Dk. Kantunzi.
Comments
Post a Comment