Ufaulu kidato cha sita watahiniwa wa skuli juu
NECTA yazuia matokeo ya watahiniwa 244
NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mtendaji Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Prof. Said Mohammed (pichani), amesema ufaulu wa watahiniwa wa skuli kwa mwaka 2025 umeongezeka kwa asilimia 0.03 huku ufaulu wa watahiniwa wa kujitegemea ukishuka kwa asilimia 2.64 ukilinganishwa na mwaka jana.
Alieleza kuwa hali ya ufaulu wa kijinsia ni sawa kati ya wanawake na wanaume kwa asilimia 93.34 na kubainisha kuwa walioshindwa kufanya mitihani kwa watahiniwa wa skuli ni 68 sawa na asilimia 0.05.
Aidha alifafanua kuwa watahiniwa wa skuli waliofaulu ni 125,779 sawa na asilimia 99.95 ya watahiniwa waliofanya mitihani, ukilinganisha na watahiniwa 103,252 sawa na asilimia 99.92 ya watahiniwa wa skuli kwa mwaka jana.
“Mwaka 2024, watahiniwa waliofanya mtihani walikuwa103,812 sawa na asilimia 99.39. Hivyo, watahiniwa wa shule waliofanya mtihani wa kidato cha sita 2025 wameongezeka kwa asilimia 21.50 ikilinganishwa na mwaka 2024”, alieleza Prof. Said.
Akizungumzia ufaulu wa wanafunzi wa kujitegemea, Prof. Said alisema kundi hilo lilikwa na watahiniwa 6,127 sawa na asilimia 90.70 ambapo katika mwaka 2024 ufaulu ulikua ni asilimia 93.34.
Akizungumzia matokeo yaliyozuiliwa, Prof. Said alisema Baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 244 wakiwemo 235 wa kidato cha sita, 4 wa mitihani ya ualimu daraja ‘A’ na watano wa stashahada ya ualimu wa sekondari.
KATIBU Mtendaji Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Prof. Said Mohammed, akizungumza na wanahabari kutangaza matokeo
Aidha alitaja sababu za kuzuiliwa matokeo hayo ni kushindwa kufanya mitihani Kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo baada ya kupata matatizo ya kiafya, hivyo watahaniniwa hao wamepewa fursa ya kufanya mitihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa mwaka ujao.
Aidha alieleza kuwa Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 71, kati yao 70 ni wanafunzi wa kidato cha sita na mmoja ni mwalimu baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu kwenye mitihani yao.
Alieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2025 kuna ongezeko la ubora wa ufaulu kwa asilimia 0.22 ambapo jumla ya watahiniwa 125,375 sawa na asilimia 99.62 wamefaulu vizuri kwa madaraja ya 1 - 3 wengi wao wakipata madaraja ya juu.
Akizungumzia ufaulu wa skuli katika makundi ya umahiri, alieleza kuwa kati ya skuli 977 zenye matokeo ya ACSEE mwaka 2025, skuli 725 (sawa na 74.21) zimepata ufaulu wa wastani wa daraja la C ikilinganishwa na madaraja mengine.
“Idadi ya shule zilizopata wastani wa Daraja la A hadi D zimeongezeka kwa asilimia 0.76 kutoka shule 921 (99.14%) mwaka 2024 hadi shule 976 (99.90%) mwaka 2025”, alieleza Prpf. Said na kuongeza kuwa hakuna skuli yenye wastani wa daraja la S au F.
Aliongeza kuwa hali hiyo inaonesha mwelekeo chanya katika matokeo ya jumla kitaifa na kwamba takwimu zinaonesha kuwa, watahiniwa wamefaulu katika masomo yote kwa kiwango cha kati ya asilimia 94.20 hadi 100 isipokuwa kwa somo la Basic Applied Mathematics ambalo ufaulu wake ni asilimia 72.66.
Kwa upande wa masomo ya Historia, Geografia, Kiswahili, Lugha ya Kiingereza, lugha ya kifaransa, Computer Science, Economics, Commerce, Accountancy na Education, zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa wamepata ufaulu wa juu ambao ni gredi A hadi C sawa na alama 60 hadi 100.
Comments
Post a Comment