Wafikieni watumishi wa ngazi za juu, viongozi waandamizi – Mhandisi Zena
NA MWANAJUMA SAID, IPA
KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena
Ahmed Said, amelitaka Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) kuwafikia
watumishi wa kada za juu na viongozi waandamizi ili kuongeza ufanisi katika
usimamizi na utoaji wa huduma za umma.
Akizungumza wakati wa mahafali ya 18 ya chuo hicho huko Tunguu, alisema kuwa kwa muda mrefu IPA inatoa mafunzo ya muda mfupi yanayolenga zaidi watumishi wa kada za chini na kati, wakati kundi la viongozi wa ngazi za juu likibaki nyuma kupata mafunzo maalum yanayohitajika katika nafasi zao pekee.
“Kuna haja sasa kuelekeza nguvu
za kuwafikia watumishi wa kada za juu na viongozi. Ni muhimu viongozi wa ngazi
zote wafikiwe kulingana na mahitaji yao ya mafunzo na upatikanaji wao”, alisema
Mhandisi Zena.
Alisema kuimarika kwa mafunzo hayo kutachochea maboresho ya mifumo ya uongozi, kuongeza uwajibikaji na kuleta matokeo chanya kwa wananchi katika taasisi za umma.
KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmeid Said, akimkabidhi Sabia Salum Abdalla, cheti cha mwanafunzi bora wakatika mahafali ya 18 yaliyofanyika ukumbi wa Dk. Ali Mohammed Shein wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu Unguja.
Aidha, aliwahakikishia wahitimu
na watendaji wa chuo kuwa Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi kwa kushirikiana na
Ofisi ya Rais – Katibu Sheria Utumishi na Utawala Bora itatoa ushirikiano wa
kutosha kuhakikisha viongozi wanapatikana na kushiriki kikamilifu katika mafunzo
yanayopangwa.
Akizungumzia eneo la utafiti na ushauri elekezi, Mhandisi Zena alisema ni lazima chuo kutoa kipaumbele, kwani ndicho chanzo cha maarifa ya kisayansi yanayowezesha Serikali kutambua na kutatua changamoto zinazolikabili taifa sasa na zijazo.
Kwa upande wa wahitimu, aliwakumbusha kuwa elimu wanayopata haina thamani endapo haitatekelezwa kwa vitendo katika maeneo ya kazi kwa kuwa mafunzo waliyoyapata ni msingi muhimu wa ujenzi wa uwezo wa kitaaluma kwa jamii na taifa.
Akisoma risala, Mkuu wa Chuo cha IPA, Dk. Shaaban Mwinchum Suleiman, alisema chuo kinaendelea kupanua wigo wa huduma kwa kuboresha ubora wa elimu na mafunzo ya uongozi.
Alieleza kuwa chuo kimeanzisha
kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Uongozi wa Rasilimali Watu (MSc in HRM),
programu ya mwaka mmoja na nusu iliyoandaliwa kukidhi mahitaji ya kuandaa
wataalamu na viongozi wenye uwezo wa kusimamia watu, kupanga mifumo ya
kiutendaji na kufanya maamuzi ya kimkakati.
“Tunataka wahitimu wetu wawe
nguzo ya mabadiliko, wenye uwezo wa kufikiri kimkakati na kuunda mifumo imara
ya uongozi,” alisema Dk. Mwinchum.
BAADHI ya Wakufunzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) wakishiriki mahafali ya 18 ya chuo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohammed Shein wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu Unguja.
Aidha aliwasisitiza wahitimu kuzingatia maadili, bidii, na kuiona elimu kama safari endelevu inayohitaji kujifunza kila wakati ili kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Baraza
la Chuo, Mmanga Mjengo Mjawiri, alisema Baraza limeendelea kusisitiza umuhimu
wa IPA kuongeza nguvu katika utoaji wa mafunzo mafupi, ambayo ni njia ya haraka
ya kuongeza ujuzi wa watumishi na kuchochea ufanisi katika utumishi wa umma.
“Tumekuwa tukihimiza chuo
kujikita kwenye mafunzo mafupi kwa kuwa ndiyo njia ya kuongeza ujuzi wa
watumishi kwa haraka”, alisema.
SEHEMU ya Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) wakiwa katika mahafali ya 18 ya chuo hicho ukumbi wa Dk. Ali Mohammed Shein wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu Unguja.
Nao baadhi ya wahitimu waliahidi
kutekeleza nasaha walizopewa na viongozi, wakisema dhamira yao ni kuendelea kujiboresha
kielimu na kitaaluma, kwa kuzingatia msemo kuwa elimu haina mwisho.
Katika mahafali hayo, jumla ya
wahitimu 786 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbali mbali, wakiwemo wanawake 474
na wanaume 312 katika programu za Astashahada, Stashahada na Shahada ya kwanza.
Comments
Post a Comment