JPM akitaka kiwanda cha mpunga kuitangaza Tanzania
NA IMMACULATE MAKILIKA, MAELEZO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
amekitaka kiwanda cha mpunga kinachozalisha bidhaa za Korie kuwa na bidhaa zenye jina la kitanzania
ili zisaidie kuitangaza nchi kimataifa.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo
mkoani Morogoro wakati akifungua kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Murzar Wilmar
Mill, kilichopo Kihonda mkoani Morogoro.
“Natoa rai kwa muwekezaji
kutengeneza bidhaa zenye jina linalohusu nchi yetu kwa sababu Tanzania tumekuwa
tukizalisha vitu vingi lakini hatutangazi nchi yetu. Siwazuii kuendelea na jina
la Korie lakini kuwe na jina jingine linalotangaza nchi”, alisema Rais
Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa
bila kuwa na viwanda hakuna uchumi, viwanda ndio sehemu pekee inayotengeneza
ajira za watanzania, na kuwa alipoingia madarakani aliamua kuhakikisha kuwa
katika kipindi cha miaka mitano Serikali inajenga jumla ya viwanda 8,477,
sambamba kufikia azma yake ya kutengeneza ajira milioni 8.
“Natoa wito kwa wizara zote
zinazohusika na uwekezaji zishirikiane katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda na
kuleta wawekezaji wa kutosha, watanzania kuwekeza hakuhitaji fedha nyingi,
tuzitumie taasisi zetu za fedha katika kuanzisha viwanda”, alisisitiza Rais
Magufuli.
Vilevile Rais Magufuli
alimpongeza mwekezaji wa kiwanda hicho
kwa kutoa ajira za moja kwa moja 75,000 na ajira nyingine zisizo za moja kwa moja kwa
wakulima, na kuongeza kuwa
Tanzania ni mahali pazuri kwa ajili ya kuwekeza na kuwa
huu ni mwelekeo muafaka wa kuingia uchumi wa kati.
Naye, Afisa Tawala wa Kiwanda
hicho, Martha David alisema kuwa kiwanda hicho
kilichojengwa kwa gharama ya dola milioni 21, kina uwezo wa kukoboa
mpunga tani 288 kwa siku, na bidhaa
zake zinazozalishwa zinauzwa nchini
pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
“Katika mwaka wa mazao 2020,
kampuni ilipokea zaidi ya tani 65,000 za mpunga kutoka mikoa mbalimbali, pia
tumetengeneza ajira za moja kwa moja kwa wananchi 75,000 na zisizo rasmi 250”, alisema Martha.
PICHANI: RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli (kushoto), akisalimiana na kiongozi wa kabila la Waluguru Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 mara baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata mazao jamii ya mikunde cha Mahashree Agro Processing, Tanzania Limited mjini Morogoro, Februari 12, 2021
Comments
Post a Comment