Mohammed Seif Khatib azikwa, Dk. Mwinyi aongoza maelfu ya wananchi

NA RAJAB MKASABA, IKULU ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi jana aliwaongoza ndugu, jamaa, marafiki na wananchi katika mazishi ya Dk. Mohamed Seif Khatib yaliyofanyika Umbuji, wilaya ya Kati.

Akisoma wasifu wa marehemu Dk. Mohamed Seif Khatib huko Umbuji, Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Khamis Abdalla Said alisema alizaliwa Januari 10 mwaka 1951 huko Umbuji, Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema Dk. Khatib ambaye kifo chake kilichotokea juzi katika Hospitali ya Al-rahma  baada ya kuugua kwa muda mfupi, ameoa na kubahatika kuwa na watoto sita.

Alisema alijiendeleza sana kielimu na  kutunukiwa shahada mbali mbali ikiwemo shahada ya Ualimu ya Chuo cha Ualimu Nkrumah Zanzibar, shahada ya  kwanza ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, shahada ya uzamili katika Sanaa na shahada ya Uzamivu ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Katika uongozi wa Vijana, Naibu katibu Mkuu huyo alisema kuwa, Marehemu alianza uzoefu wa kazi kama Mwalimu wa Skuli mbali mbali ikiwemo skuli za msingi, sekondari, mkufunzi Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni na Mhadhiri wa muda, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Alisema aliongoza wizara mbali mbali kuanzia mwaka 1988 hadi 2010, ambapo aliwahi kuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Ofisi ya Makamu wa Rais anaeshughulikia Mambo ya Muungano, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na Waziri  , Ofisi ya Waziri Mkuu (Habari na Siasa).

Katika wasifu huo, Naibu huyo alisema marehemu alikuwa mzoefu katika siasa kwani aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Uzini kuanzia mwaka 1988 hadi 2015, Mjumbe wa NEC, CCM kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 2017, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa CCM (Idara ya Siasa na Uenezi kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2017.

Sambamba na hayo, kwa maelezo ya Naibu katibu Mkuu huyo, marehemu ameandika vitabu mbali mbali kama vile, Fungate ya Uhuru, Wasaka Tonge, Utenzi wa Ukombozi, Chanjo, Vifaru Weusi na Kipanga ambapo pia, ana miswada ambayo haijachapishwa.

Pia, alisema kuwa Marehemu amesimamia wanafunzi wa Uzamili na Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Dodoma na kutunga  nyimbo mbali mbali  za taarabu na  kuandika makala nyingi za kiswahili.

Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba  marehemu alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar kuanzia mwaka 2014 hadi kufariki kwake lakini pia, alikuwa mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi Serikali.

Katika wasifu huo pia, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Marehemu alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo waliochukua Uzamivu (PhD ya Kiswahili) hapa nchini.

Hapo jana asubuhi viongozi na wananchi walihudhuria katika sala ya kumuombea marehemu huyo iliyofanyika katika msikiti Noor Muhammad (S.A.W), Mombasa kwa Mchina.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, Rais mstaafu Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili mstaafu Balozi Seif Ali Idd na  viongozi kutoka serikalini na vyama vya siasa.

MAELEZO YA PICHA JUU:

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akiweka udongo katika kaburi la marehemu Mohammed Seif Khatib, wakati wa mazishi yake yaliyofanyika jana kijijini kwao Umbuji wilaya ya Kati. (PICHA NA IKULU).


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango