Kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani: SMZ yatoa bei elekezi bidhaa za vyakula
NA MWANDISHI WETU
WAKATI waislamu wa Zanzibar
wakitarajiwa kuungana na wenzao duniani kote kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa
Ramadhani, serikali imewaonya wafanyabiashara watakaopandisha bei za vyakula
hususani vinavyotumika kwenye mfungo huo.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake Darajani,Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda
Zanzibar, Omar Said Shaaban (pichani), alisema watakaopandisha bei hizo watachukuliwa
hatua kali za kisheria.
“Mimi binafsi nitazunguka katika maeneo
mbalimbali ya biashara kujiridhisha kama kweli wafanyabishara wanafuata
maeekezo ya serikali na ijulikane kwamba zipo adhabu kali kwa watakaokiuka
taratibu,” alisema.
Ili kuhakikisha bei
hazipandi, Waziri Shaaban alisema wameunda kikosi kazi kinachoshirikisha Tume
ya ushindani kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kuchukua hatua
zinazostahili.
Licha ya sheria ya ushindani
na kumlinda mlaji namba tano ya mwaka 2018 kutobainisha adhabu anazotakiwa
kuchukuliwa anaekwenda kinyume, Waziri huyo alisema faini watakayotozwa inaweza
isiwe chini ya shilingi milioni moja.
“Kumekuwepo na tabia ya muda
mrefu ya baadhi ya wafanyabiashara wenye tamaa kutumia fursa ya mwezi mtukufu
kupandisha bei kiholela hasa kwa bidhaa muhimu kama mchele, sukari na
ngano. Tabia kama hizi kutaka kuchuma
faida kupitia mgongo wa wanaofunga hazikubaliki na mara nyingi husababisha
wananchi wenye wa maisha duni kutekeleza ibada yao ya funga katika mazingira
magumu,” alisema
Kuhusu kupunguza kodi za
bidhaa kama ambavyo huwa inafanyika kila mwezi mtukufu, Shaabani alisema safari
hii hawajaondoa kodi kwa sababu inaonekana hata serikali inapoondoa kodi hizo
wafanyabiashara huwa hawashushi bei.
Katika mkutano huo Waziri
huyo alitangaza bei elekezi ya bidhaa za mchele, ngano na sukari.
Alisema mchele wa mapembe
utauzwa kwa shilingi 1,600 kwa kilo, sukari shilingi 2,000 kwa kilo na unga wa
ngano utauzwa shilingi 1,600 kwa kilo.
“Bei hizi zitabaki hivyo
kwenye masoko mpaka hapo zitakapofanyiwa mapitio na kutangazwa vyenginevyo na
serikali,” alisema.
Naye mfanyabiashara maarufu
visiwani humu Mohamed Raza, alisema wanaopandisha bei za vyakula hawana huruma
na wananchi akidai bei
za vyakula na kodi bado
hazijapanda.
“Lazima tuwarahisishie wananchi kujikimu,
waweze kula futari sio sisi (wafanyabiashara) kutumia fursa hii kuwakomoa,
ushuru bao upo vilevile bei sokoni inakubalika ipo vilevile, tuwasaidie
wananchi wapo wanaokula mlo mmoja kwa sababu hawana uwezo,” alisema.
Comments
Post a Comment