HOTUBA YA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA YA KUSAINI HATI ZA KUONDOA HOJA ZA MUUNGANO ZILIZOPATIWA UFUMBUZI
TAREHE 24 AGOSTI, 2021- ZANZIBAR
Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Waheshimiwa Mawaziri wa SMT na SMZ,
Waheshimiwa Naibu Mawaziri wa SMT na SMZ,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali – SMT, SMZ
Katibu Mkuu Kiongozi - SMT, SMZ
Makatibu Wakuu - SMT, SMZ
Wanahabari,
Mabibi na Mabwana.
Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania!
Ndugu Wajumbe, naomba nianze kwa kufuata mfano wa wenzangu
walionitangulia, kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukutana hapa
tukiwa na afya njema katika siku hii muhimu kwa mustakabali wa Muungano wetu. Ningependa
pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan kwa kunikabidhi kijiti hiki cha kusimamia masuala ya Muungano, akiwa ameacha
msingi mzuri wa kuendelea kutafutia ufumbuzi changamoto za Muungano.
Aidha, napenda kutumia fursa
hii kuwashukuru kwa dhati wajumbe wote wa kikao hiki kwa kazi kubwa na ushiriki
wenu mzuri katika vikao vya wataalam kuhakikisha changamoto zinazoukabili Muungano
wetu zinatafutiwa ufumbuzi. Nafahamu haikuwa rahisi kufanya hivyo, ila kwa kuwa
mna ari na nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa Muungano wetu adhimu na adimu
unadumishwa na kustawi kwa kila hali, ndio maana leo hii tumeweza kutatua
changamoto kumi na moja (11) ndani ya kipindi cha miaka miwili, ambapo hoja tisa
(9) zimeandaliwa hati za makubaliano na kusainiwa leo na hoja mbili (2) ni za
kiutendaji ambazo hazihitaji kuandaliwa hati. Nawapongeza sana.
Ndugu Wajumbe, hafla hii ni muhimu sana kwani ni uthibitisho thabiti kuwa, Kamati
hii inafanya kazi kubwa sana katika kulinda na kuimarisha Muungano wetu kwa
kuhakikisha kwamba, wananchi wa pande zote mbili za Muungano wananufaika na
matunda ya Muungano wetu.
Hii pia inatoa fursa kwa
wananchi kuwa na uelewa mpana kuhusu jitihada mbalimbali ambazo zinachukuliwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kutatua changamoto za Muungano.
Ndugu Wajumbe, tukio hili linafanyika
kwa mara ya tatu, mara ya kwanza lilifanyika hapa Zanzibar tarehe 2 Juni, 2010
Salama Hall, Bwawani na mara ya pili tarehe 17 Oktoba, 2020 katika Ikulu
ya Dar es Salaam. Nina imani utaratibu huu ulio ndani ya mwongozo wetu utaongeza
ari na hamasa kwa pande mbili za Muungano kuzidisha ushirikiano na hatimaye kuulinda
na kuudumisha Muungano wetu. Makubaliano
yaliyofikiwa leo yatakuwa na faida zifuatazo kwa pande zote za Muungano:-
Moja, kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza
Uvuvi wa Bahari Kuu, Sheria Na. 5 ya mwaka 2020 kutaongeza ufanisi katika
usimamizi na uendelezaji wa uvuvi wa Bahari Kuu na kuhamasisha uwekezaji katika
uvuvi wa Bahari Kuu.
Pili,
makubaliano juu ya usimamizi na mgawanyo wa ajira katika Taasisi za Muungano
yataongeza hamasa na manufaa kwa wananchi wa pande mbili za Muungano kutumia
fursa zilizopo katika Muungano wetu;
Tatu, makubaliano
juu ya utaratibu wa mgawanyo wa
mapato yatokanayo na misaada ya kibajeti kutoka nje (GBS) na misaada ya kibajeti
ya kisekta yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
Nne, kusainiwa kwa Mkataba wa Mkopo wa Fedha za Mradi
wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kutaimarisha huduma za afya kwa
wananchi wetu;
Tano, kusainiwa
kwa Mkataba wa Mkopo wa Ujenzi wa Barabara ya Chake Chake hadi Wete – Pemba kutaimarisha huduma za kijamii kwa kurahisisha
mawasiliano na kuharakisha maendeleo ya nchi;
Sita, kupitiwa
kwa gharama za ujenzi wa mradi wa Bandari ya Mpigaduri na kubaini kuwa gharama
hizo ni kubwa sana, hivyo, SMZ kufanya uamuzi wa kuvunja mkataba na CHEC ni
jambo la busara sana ambalo limeepusha nchi kuingia kwenye hasara;
Saba, kufanya maboresho ya
Mfumo wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye huduma za simu kumeondoa malalamiko
kutoka kwa Makampuni ya simu na kunaimarisha mazingira ya uwekezaji;
Nane, ni
jambo la busara sana kuruhusu mapato yanayotokana na Tozo za VISA kutumika pale
yalipokusanywa kama ilivyo kwenye mapato mengine ya Muungano; na
Tisa, Makubaliano ya uingizaji wa maziwa ya AZAM katika soko la
Tanzania Bara yanaondoa malalamiko ya mwekezaji lakini pia kuendelea kuimarisha
biashara na ajira nchini.
Ndugu Wajumbe, Nia na Madhumuni ya haya
yote ni kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu. Napenda nitumie fursa
hii kutoa rai kwa taasisi zote husika kuwa, changamoto zinazoendelea kutafutiwa
ufumbuzi na zile zitakazojitokeza, ni muhimu kuzitambua mapema, kuzijadili kwa
uwazi na umakini ili kuzitafutia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote mbili za
Muungano. Hivyo, ni imani yangu kuwa kusainiwa kwa Hati hizi leo, kutaongeza
tija na hamasa ya kutafuta ufumbuzi wa hoja zilizobakia kwa ustawi wa Muungano
wetu.
Ndugu Wajumbe, nawapongeza tena kwa
jitihada za kuhakikisha Muungano wetu adimu na adhimu unaendelea kuimarika. Tuongeze
jitihada katika kuzitafutia ufumbuzi hoja zilizobakia ambazo zipo katika hatua
mbalimbali za kuzitafutia ufumbuzi. Naziagiza Wizara za Fedha na Mipango za SMT
na SMZ kuchukua jitihada za makusudi kuzitafutia ufumbuzi hoja zinazohusu
ushirikiano katika masuala ya fedha ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.
Aidha, nasisitiza kwa sekta zote
kuendeleza vikao vya kisekta kwa pande zote mbili za Muungano ili kupunguza
hoja zinazoletwa kwenye kamati ya Pamoja.
Ndugu Wajumbe, baada ya maneno haya
machache natamka rasmi kuwa, hoja za Muungano kumi na moja (11) zilizopatiwa
ufumbuzi zimeondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
Comments
Post a Comment