Kamati TASAF yatakiwa kuzitembelea kaya za wanufaika

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama ameitaka Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwa na utamaduni wa kuwatembelea walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Hatua hiyo imetajwa itawasaidia kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa mpango huo ambao serikali inautekeleza kwa lengo la kuimarisha maisha ya kaya maskini nchini.

Jenista alitoa maelekezo hayo jijini Dodoma, wakati akizindua Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF iliyoteuliwa hivi karibuni mara baada ya kamati iliyopita kumaliza muda wake.  

Aliwahimiza wajumbe wa kamati hiyo, kuhakikisha wanazungumza na viongozi, waratibu na walengwa katika maeneo yote ambayo mpango unatekelezwa ili kufikia lengo la serikali la kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la umaskini.

“Mwenyekiti na wajumbe wa kamati hii, tembeleeni maeneo ambayo mpango wa TASAF unatekelezwa ili mjiridhishe namna ambavyo unawafikia walengwa na kuwanufaisha,” Jenista alisisitiza.

Jenista aliongeza kuwa, wajumbe wa kamati wakitembelea maeneo ambayo mpango wa TASAF unatekelezwa, watapata fursa ya kujionea namna walengwa walivyonufaika, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ambazo walengwa hao wa TASAF wanakabiliana nazo.

Jenista alisema kuwa serikali chini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan haitomuacha mtu nyuma kufikia malengo ya maendeleo kama yalivyoainishwa katika dira ya maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Ilomo amemhakikishia, Jenista kuwa yeye pamoja na kamati yake watayafanyia kazi maelekezo yote ambayo ameyatoa ili kutimiza lengo la serikali la kuboresha maisha ya kaya maskini.


Naye, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dk. Moses Kusiluka alisema, ataendelea kushirikiana na TASAF ili kuhakikisha inatimiza lengo lake la kuboresha maisha ya wananchi ambao wanaishi katika familia zenye hali duni kiuchumi.


Mapema akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake, Mkurugenzi Mtendaji , Ladislaus Mwamanga alisema TASAF imekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya kaya maskini ikiwa ni pamoja na kujenga rasilimali watu ya kutosha kwa kuwawezesha kielimu wanafunzi wanaotoka kwenye kaya maskini kutoka hatua moja kwenda nyingine.

“Mwaka jana, TASAF kwa kushirikiana na bodi ya mikopo tumewawezesha wanafunzi 1200 kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini, na mwaka huu mchakato bado unaendelea lakini tunatarajia kuwawezesha wengi zaidi kwani walioomba wako zaidi ya 3000,” Mwamanga alifafanua.

Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa sasa inaundwa na Mwenyekiti Peter Ilomo, pamoja na wajumbe wengine ambao ni Balozi Zuhura Bundala,  Richard Shilamba, Dkt. Charles Mwamwaja, Dkt. Ruth Lugwisha, Dk. Naftali Ng’ondi, Ali Salim Matta, Mhandisi Rogatus Mativila na Dk. Grace Magembe.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango