TEWW yawafikia wasichana 3,333 walioshindwa kuendelea sekondari

 NA SAIDA ISSA, DODOMA

TAASISI ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imefanikiwa kuwafikia wasichana 3,333 walioshindwa kuendela na masomo ya sekondari kutokana na mazingira magumu, kupata ujauzito na ndoa za utotoni.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dk. Emanuel Ng'umbi (pichani) ambapo alisema kuwa idadi hiyo ni sawa na asilimia 111 ya lengo ambapo waliendesha mafunzo kwa nyakati tofauti kwa wasimamizi na watendaji, wawezeshaji na walimu wa madarasa ya mradi wa SEQUIP.

"Kwa mwaka 2022/2023, TEWW itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Tekonolojia kuandaa Juma la Elimu ya Watu Wazima, vile vile TEWW itahamasisha, kusajili na kufundisha wanafunzi 3,000 wa mradi wa SEQUIP kwa mwaka 2023," alisema.

Aliongeza kuwa  TEWW inatarajia kupanua mpango wa IPOSA katika mikoa mipya sita ya Tanzania bara kwa kujenga karakana za kufundishia na kupanua mafunzo ya TEHAMA kwa wanafunzi wa IPOSA.

“Kwa upande wa programu ya IPPE, TEWW inatarajia kuanza kusajili vituo vya mafunzo vitakavyotumia mtaala ulioboreshwa wa IPPE,” alieleza Dk. Ng'umbi.

Alieleza kuwa TEWW imekusanya takwimu za hali ya kisomo kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na inaendelea na uchambuzi wa taarifa na takwimu hizo ikiwa ni hatua ya mwanzo ya utafiti wa hali ya kisomo na elimu kwa umma nchini.

Alifafanua kuwa katika kuimarisha miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji Katika mwaka 2021/2022, kwa kupitia mradi wa SEQUIP, TEWW ilikarabati majengo ya ofisi na madarasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Ruvuma, na Dodoma pamoja na kuanza ujenzi wa majengo ya ofisi na madarasa katika mikoa minne ya Pwani, Rukwa, Iringa na Manyara.

“Jumla ya shilingi bilioni 1.2 kimetumika, pia TEWW ilianza ujenzi wa jengo la utawala katika kampasi ya Morogoro kwa kutumia fedha kutoka serikali kuu ambapo kiasi cha shilingi milioni 500 kilitolewa na serikali kuu kwa ajili ya kazi hiyo kwa mwaka 2021/2022,” alifafanua.

Alisema katika mwaka wa 2022/2023, TEWW inatarajia kuendelea na ujenzi wa madarasa na ofisi katika vituo vya mikoa sita na ukarabati katika vituo vya mikoa miwili.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ni Taasisi ya umma iliyoanzishwa chini kwa sheria ya bunge namba 12 ya mwaka 1975 ikiwa ni taasisi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo jukumu la TEWW  kusimamia elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango