Changamoto sekta ya habari kupatiwa ufumbuzi

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAM


SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kuwa itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wa habari katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili zikiwemo sheria zisizo rafiki zinatatuliwa.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alieleza hayo hivi karibuni alipokua akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), uliofanyika jijini Dar es salaam.

Alisema serikali itafanya kazi na waandishi kwa sababu inatambua mchango wa UTPC katika kunyanyua uwezo wa waandishi wa habari hapa nchini, kuwezesha ofisi za waandishi wa habari mikoani kufanya kazi, kuchochea maendeleo mikoani na kupasha habari wananchi waweze kupata uelewa ili kufanya uamuzi sahihi

“Niko tayari kufanya kazi na UTPC wakati wa shida na raha ninachowaomba msiniangushe mniunge mkono na mimi nitawaunga mkono waswahili wanasema imani huzaa imani, mimi nina imani kubwa na UTPC na ninapenda sana umoja huu kwa sababu ninatambua hapa nilipo ndipo mahali sahihi kwa kuwagusa waandishi wa habari wote bila kujali maeneo walipo,” alisema.

Alieleza kuwa moja ya changamoto zinazoikwaza tasnia ya habari ni sheria zinazohitaji kurekebishwa hivyo alihakikisha dhamira ya serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari kufanya kazi katika mazingira yote ambapo alisema wizara ya habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria ili wabunge wakiridhia tuendelee na utekelezaji wake.

Wajumbe na waalikwa wakifuatilia hotuba

Msigwa alishauri UTPC kutengeneza mazingira ya kuvutia wawekezaji katika habari kwani hivi sasa vyombo vya habari vingi havilipi mishahara, pia vingi hakuna mikataba ya waandishi wa habari.

“Tunatakiwa tujenge mazingira ambayo watakuja wawekezaji ambao wataona hapo ni mahali pa kuwekeza ili wakiwekeza walipe mishahara,” alisema.

Alisema Klabu za waandishi wa habari zinatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taaluma ya uandishi wa habari pamoja na kuchangia maendeleo ya mikoa mbalimbali nchini.

Wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa UTPC kutoka klabu za Tanga, Njombe na Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa SJMT, Gerson Msigwa (wa nne kulia) baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo.

“Natoa wito kwa mamlaka mbali mbali za serikali kutosita kuchangia vilabu vya waandishi wa habari wa mikoa isiwe ni kuwakumbuka wakati wa matukio pekee bali kwa wakati wote ikiwemo kipindi ambacho mnatenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza shughuli ambazo mnatambua kuwa zitawashirikisha waandishi wa habari,” alisema.

Awali Rais wa UTPC, Deogratius Nsokolo, alisema kuna klabu 28, kati ya hizo 26 zipo bara na mbili zipo Zanzibar lengo likiwa ni kuhakikisha waandishi wanakua na mazingira wezeshi na salama katika utekelezaji wa majukumu yao.

Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo

Alisema mkutano huo utakuwa chachu ya kuongeza ufanisi, kuwasemea wasio na sauti, kukosoa pale panapotakiwa na kusifia pale panapotakiwa kusifiwa.

Alisema lengo lililopo sasa ni kuimarisha Klabu za waandishi wa habari Dodoma na Dar es Salaam, ikiwezekana makao makuu ya UTPC yahamishiwe makao makuu ya nchi ili kuwa karibu na viongozi wa serikali na rahisi kufikika na wadau wa habari.

 

Aidha katika mkutano huo, wajumbe walipitisha maazimiombali mbali likiwemo la kuhamisha makao makuu ya taasisi hiyo kutoka Mwanza hadi Dodoma ili kurahisisha mawasiliano na taasisi mbali mbali za serikali na binafsi.

 

Mkurugenzi Mstaafu wa UTPC Aboubakar Karsan

Akizungumza wakati wa hafla ya kumuaga iliyoenda sambamba na mkutano huo, aliyekua Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Aboubakar Karsan, aliwashukuru viongozi wa klabu na UTPC kwa ushirikiano waliompa wakati wa utumishi wake.
 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango