Dk. Mwinyi ahimiza malezi bora ya watoto, vijana

NA MWANDISHI MAALUM, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameihimiza jamii kuweka mkazo kwenye malezi ya watoto na vijana ili kukuza taifa lenye maadili, nidhamu na kizazi chema chenye kumjua Mwenyezi Mungu.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu Zanzibar 1445 Hijria yaliyofanyika katika Masjid Munawwara, Mfikiwa  mkoa wa Kusini, Pemba.

Alisema ni wajibu wa wazazi na walezi kuwasimamia vyema watoto wao na kuwapa elimu ya dini na dunia ili kuwaepusha na vitendo vya uvunjivu wa amani, tabia mbaya na vitendo vya udhalilishaji.

Akizungumzia historia ya tarehe ya Kiislaam, Alhajj Dk. Mwinyi alieleza ilianza mara baada ya  Mtume SAW kuhama Makka na kuhamia Madina ambako utulivu na Amani ulipatikana na kuwa chanzo cha kuenea uislam dunia nzima.

Alisema lengo la kuadhimishwa mwaka Mpya wa Kiislam 1445 H ni kuendelea kusisitiza na kuhimiza amani, ushirikiano na upendo kwenye jamii Katika kutekeleza mambo ya heri.

Aidha, aliendelea kuhimiza umoja na mshikamano kwenye jamii ili nchi izidi kupata neema na baraka kutoka kwa Mola.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alipongeza ushirikiano uliopo baina viongozi wa Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba na viongozi wa Chama, katika kutela Maendeleo ya kisiwa hicho.

Akiwasilisha mada ya nidhamu ya kodi kwenye kongamano la mwaka mpya wa kiislaam 1445, Sheikh Said Ahmad aliwataka watumishi wa umma kuutumia vyema muda wao wanapotekeleza majukumu yao ili kukwepa kuchuma mali za dhulma zinazotokana na utumishi waa hasa kwenye ibada zao.

Aidha alihimiza umuhimu wa kulipa Kodi kwa serikali kwa mujibu wa sheria za Kiislam ambapo Sheikh  Izud Alaw kutoka Mombasa Kenya,  aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislam juu kuzingatia vyema tarehe za kiislam kwenye mfumo wa maisha yao.

Vile vile, aliwataka waumini kutofungamana na kufuatilia masuala na muandamo wa mwenzi na hitilafu za Arafa pekee, bali waangalie mambo mengine muhimu ikiwemo suala la eda kwa mwanamke alieacha ama kufiliwa na mumewe kwa tarehe zinapoanza hadi kumalizika kwake.

Akiwasilisha taarifa ya maadhimisho hayo, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti, Sheikh Khalid Mfaume, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuitangaza tarehe ya kiislam na kuendeleza historia ya dini walioiacha maulamaa na kuahidi Ofisi ya Mufti inajukimu ya kuendelea kuitangaza na kuishajisha kwa jamii.

Alisema maadhimisho hayo yanayofikia kilele leo, yalitanguliwa utoaji wa huduma za matibabu ya macho, dua ya kuliombea taifa, kongamano la wanawake wa Kiislamu lililohudhuriwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Hajjat Dk. Samia Suluhu Hassan, maonesho ya biashara yaliyowashirikisha wafanyabiasha wadogo na wajasiriamali, matembezi ya ZAFA yatakayofanyika kisiwani Pemba  yaliyolenga kuboresha afya pamoja na matembezi ya hiari yatafanyika Unguja.

 


Comments

Popular posts from this blog

Balozi Mpanda ahimiza ubunifu uhifadhi wa mazingira

Vodacom yawapa uhakika wa matibabu mama, watoto wachanga