Dk. Mwinyi ahimiza matumizi nishati salama
Apongeza ushirikiano wa Oryx, Vigor uwekezaji mradi wa gesi
NA MWANDISHI MWAALUM
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezipongeza kampuni
za Oryx Gas Tanzania Ltd na kampuni ya TP Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Vigor Turky’s Group of
Companies kwa kujenga bohari ya kwanza ya kuhifadhi nishati ya gesi ili
kuongeza usambazaji wa gesi ya iliyokandamizwa visiwani humo.
Akihutubia wananchi wa Zanzibar baada ya kuzindua bohari hiyo huko Mangapwani, mkoa wa Kaskazini Unguja Dk. Mwinyi alieleza hatua hiyo itachochea utekelezaji wa mkakati wa taifa wa ulinzi wa mazingira na ongezeko la matumizi ya nishati safi kwa shughuli mbali mbali.
Alieleza uwepo wa
bohari ya kuhifadhi gesi pamoja na miundombinu mingine ni sehemu ya utekelezaji
wa mradi wa bandari jumuishi inayojengwa katika ukanda huo ambayo itahusika bandari
ya meli za mafuta, gesi pamoja na shughuli nyingine.
Alisema kuanzishwa kwa bohari ya kuhifadhi ya gesi Zanzibar kutaongeza chachu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na hivyo kufikia malengo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwamba ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya wananchi itumie nishati safi ya kupikia huku akisisitiza umuhmu wa bei ya gesi kupunguzwa ili wananchi wengi watumie.
“Kwa muda mrefu
tulikuwa tunamia bandari ya Malindi lakini kutokana na ongezeko la shughuli za
kiuchumi bandari ile haitoshi, hivyo Serikali ilitangaza eneo la Mangapwani
kuwa bandari kwa ajili ya nishati ya gesi, mafuta na miundombinu mengine”,
alieleza Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa; “Sasa tutakuwa tunapokea meli kubwa za gesi na kuhifadhiwa katika matanki mawili makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi tani 130 yaliyojengwa na Oryx. Hivyo niziombe kampuni nyingine kufuata nyayo za Oryx kwa kujenga miundombinu yao katika eneo hili”.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Limited, Benoît Araman, alisema
kufunguliwa kwa bohari hiyo kunathibitisha dhamira ya kampuni ya Oryx Energies ya
kuwekeza katika miundombinu muhimu inayosaidia matumizi salama na mapana ya
gesi nchini Tanzania.
“Pia hatua hii inakidhi
ombi la serikali la kuhakikisha usambazaji endelevu wa LPG kila mahali nchini. Soko
la gesi la Tanzania limeshuhudia ongezeko la uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa
karibu mara 13 katika muongo uliopita, kutoka tani 20,000 mwaka 2010 hadi tani
293,000 mwaka 2023”, alieleza Amaran.
Aliongeza kuwa Oryx
Gas Zanzibar imeungana na kampuni ya TP Limited yenye makao yake Zanzibar
ambayo ni kampuni tanzu ya Vigor Turky’s
Group of Companies (Vigor Group), kujenga bohari hiyo ya kimkakati na kuongeza usambazaji wa gesi ya LPG visiwani
humo.
“Mkataba huu unaonesha kujitolea kwa Oryx Energies katika kuendeleza ushirikiano na makampuni ya wazawa.Bohari ya Mangapwani, ambayo ilianza kufanya kazi mapema Mei ina uwezo wa kuhifadhi tani 1,300 za gesi ya LPG, na ilipokea meli yake ya kwanza ya tani 1,200 mnamo Mei 2, 2024”, aieleza.
“Kusaidia Mpango wa
matumizi wa nishati safi ya kupikia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Gesi ya
LPG inazidi kuwa sehemu muhimu ya mchanganyiko wa matumizi ya nishati
mbalimbali za kupikia Zanzibar, ikishughulikia mahitaji ya kaya, biashara, na
sekta ya utalii inayokua kwa kasi”alisema.
Awali Mwenyekiti wa kampuni za Vigor Taufiq Salim Turky alisema wameungana Oryx kwa kutambua uwezo walionao miaka mingi katika soko la gesi nchini hivyo ni imani yao sasa gesi itapatikana kwa wengi na kwa bei nafuu.
Alisema mpango wao
ni kupunguza bei ya gesi Zanzibar kwa asilimia 20 kuanzia Julai 1, mwaka huu na
baadae kupungua bei kwa asilimia 30. “Hivyo Oryx Gas wameiweka bohari hii
katika viwango vya kimataifa.
“Bohari hii
inamilikiwa na Vigor kwa asilimia 100, lakini kwa uendeshaji tumamua kuwapa
wenzetu wa Oryx .Uendeshaji tumeukabidhi kwa Oryx kwa kuamini wao ni kinara
katika soko la Tanzania.Wakati tunaanza huko nyuma soko lilikuwa ni tani tatu
lakini sasa soko lao limekuwa na kufikia tani 800”, alisema.
Aliongeza kuwa; “Hata hivyo alisema ni asilimia 12 tu ndio wanaotumia gesi Zanzibar na upande wa Tanzania bara ni asilimia 9 hivyo safari safari bado ndefu”.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Omar Ali
Yussuf, alisema kwa miaka mingi sekta ya nishati hasa gesi, walikuwa wanatumia
bandari ya Malindi lakini sasa wamepeta bandari ambayo itashusha gesi, mafuta
na itatumika kwa shughuli nyingine kwenye hilo la Mangapwani.
“Kabla ya kuwepo kwa bandari hii ya kushusha gesi na mafuta tulikuwa tunatumia majahazi na vyombo vingine ambavyo havina salama lakini kwa maelekezo ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi leo tumeweza kuwa na bandari kwa ajili ya meli zenye gesi na mafuta” alisema.
Alisema kwa kupitia
mipango ya serikali pamoja na sera nzuri za uchumi wa buluu watahakikisha
bandari ya Mangapwani wanataka iwe kituo kikuu cha kusafirisha gesi na mafuta
kwa ukanda wa Afrika Mashariki huku akifafanua kuwa bei ya nishati ya mafuta na
gesi kwa Zanzibar iko chini ukilinganisha nchi nyingine.
Comments
Post a Comment