Silaa azindua mnara wa mawasiliano ya simu Makuru
NA SAIDA ISSA, SINGIDA
WAZIRI
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amezindua mnara wa
mawasiliano ya simu uliojengwa katika kijiji cha Hika, kata ya Makuru, wilayani
Manyoni Singida.
Waziri Silaa aliongeza
kwa kusema kuwa, dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk. Samia
Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini yanafikiwa na huduma bora
za mawasiliano ikiwemo mtandao wa intaneti.
"Dhamira yetu
ya kimkakati ya kuimarisha muunganisho katika maeneo ya vijijini na sasa
tunafanya uboreshaji mkubwa wa minara ya mawasiliano inayofanya kazi kutoka
teknolojia ya 2G kwenda 3G/4G", alisema.
Kwa upande wake
Mkuu wa mkoa wa Singida, Halima Dendego, aliishukuru serikali na kuongeza kuwa,
sasa wananchi wa Kata ya Makuru na vijiji vyake wanaweza kutumia mawasiliano ya
simu kuboresha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Aliongeza kuwa, gharama
ya jumla ya ujenzi wa manara huo ni shilingi milioni 272 kati ya hizo UCSAF
imetoa ruzuku ya shilingi milioni 118 na TTCL imetoa zaidi ya shilingi milioni
150 ambapo takribani wananchi 24,000 katika kijiji cha Hila, Londoni na
Msemembo na vijiji vya jirani watanufaika na kuwepo kwa mnara huo.
Waziri Silaa yuko
mkoani Singida kwa ziara ya siku tano yenye lengo la kukagua, kutembelea na
kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, kauli mbiu ikiwa ni; ‘Rais Samia na
maendeleo, wasikie na waone’.
Comments
Post a Comment