Maafisa Habari Z'bar watakiwa kuongeza kasi ya uwajibikaji
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amewataka Maofisa Habari na Mawasiliano wa wizara na taasisi za serikali kutekeleza majukumu yao vyema na kutoa taarifa za utendaji wa serikali kwa wananchi.
Waziri Tabia alieeleza hayo jana katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni, mjini Unguja wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Maafisa Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICCO) na kusema maafisa hao na watu binafsi wana jukumu la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata habari za taasisi zao kwa wakati na usahihi.
"Kuna miradi mingi ya maendeleo inafanyika katika taasisi zenu lakini wananchi hawaelewi kutokana na taasisi hizo kukaa kimya bila kuijulisha jamii", alisema Waziri Tabia.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu 18 (1 na 2) kinatoa uhuru kwa kila mtu kuwa na haki ya kupokea na kutoa habari na kinaonesha haki ya raia kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio yanayofanyika nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi.
Alifahamisha kwamba kuwepo kwa jumuiya hiyo kutasaidia kutekeleza malengo ya kuundwa kwake ili jamii ipate taarifa ya maendeleo yanayotekelezwa na serikali yao sambamba na kupata fursa ya kuzieleza changamoto zao.
Aidha alitoa wito kwa viongozi wa taasisi za serikali kuwashirikisha ipasavyo Maafisa Habari wa taasisi zao katika vikao vya kiutendaji kwani kutofanya hivyo kunachangia kuwadumaza na wananchi kutopata taarifa.
"Kuna miradi bado haijatangazwa kwa wananchi ili kuitambuwe ikiwemo Vwanja vya mpira,Bandari, barabara, barabara za juu (flyover), na kwengine mwingi lakini hamtangazi kwa jamii wakajuwa", aliesema Mbeto.
Kwa upande wa Katibu wa Jumuiya ya Maafisa wa Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICOO), Makame Khamis Mohamed, alisema lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuwaweka pamoja maafisa habari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania ili kuimarisha umoja, uwazi na uwajibikaji kupitia Wizara zao, sambamba na kuongeza umahiri na uweledi katika kazi zao.
Hata hivyo amefahamisha kuwa
kutokana na hali ya Maofisa Habari katika taasisi haiendani na hali ya sasa
ambayo inaviza utekelezaji wa majukumu sambamba na kupatiwa mafunzo ya mara kwa
mara yatasaidia kuongeza weledi wa kazi zao.
Comments
Post a Comment