Tangazeni kazi zenu kupitia vyombo vya habari - Dk. Mzuri

NA NAFDA HINDI, TAMWA

WANAWAKE nchini wamehimizwa kuvitumia vyombo vya habari ipasavyo kutangaza kazi na shughuli wanazozifanya katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake viongozi kupitiaMradi wa Wanawake na Uongozi katika kukabiliana na mabadilio ya tabianchi  (ZanzAdapt),  Mkurugenzi wa chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ), Dk. Mzuri Issa Ali, alisema wanawake wanafanya mambo mengi katika jamii ila bado mchango wao haujatambulika kama ilivyo kwa wanaume.

Hivyo alieleza kuwa kwa kutumia vyombo vya habari kutawezesha kutambulika na kujitangaza kwa haraka hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Alisema historia ya Tanzania na Zanzibar  haioneshi kwa kiasi kikubwa mchango wa wanawake kwa sababu wanawake wengi bado hawajawa na ujasiri na uthubutu wa kutumia vyombo vya habari kwa usahihi.

“Wanawake wanafanya mambo mengi katika jamii na kujitoa zaidi, sasa wakati umefika kueleza changamoto na mambo yanayowahusu kupitia vyombo vya habari ili kupatiwa ufumbuzi,” Dk. Mzuri.

Naye Mkufunzi katika mafunzo hayo, Sophia Ngalapi, alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutatua changamoto za kijamii zinazowakabili kwa mamlaka husika kuzitafutia ufumbuzi ikiwa jamii itapaza sauti zao.

‘’Kupitia vyombo vya habari nyinyi ni mashahidi tuanaona hatua zinazochukuliwa kwa wahusika  endapo kutatokezea tatizo”, alieleza Ngalapi.

Akizungumzia usawa wa kijinsia alisema wazazi na walezi wanapaswa kuwalea watoto wao katika muktadha wa kijinsia kuhakikisha kila mtoto anapata fursa na haki sawa kama zilivyoeleza katiba zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bila kujali jinsia zao.

Naye Afisa Mawasiliano kutoa Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP), Munira Iddi Kaoneka, alisema wanawake hawana budi kujiamini na kutumia vyombo vya habari kutangaza kazi wanazofanya ikiwemo mitandao ya kijamii kwani ujumbe wao hufikia watu wengi na kwa wakati mmoja.

“Mukilima na kuvuna mazao yenu halafu mukanyamaza kimya nani atajuwa kama muna bidhaa, ila chukuwa video ukivuna mazao kisha rusha Tiktok weka nambari za simu, soko litakuja na watu watakutafuta, alieleza Munira.

Nao Wanawake viongozi waliopata mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuwainuwa kiuchumi kwa kulima kilimo msitu chini ya mradi wa ZanzAdapt wamesema watayatumia vyema mafunzo hayo kwa kuwa mabalozi bora wa kuwafunza wengine il kukabiliana na mbadiliko ya tabianchi.

Mradi wa Wanawake na Uongozi katika kukabiliana na mabadilio ya tabianchi  (ZanzAdapt) unatekelezwa kwa pamoja na Chama cha Waandishi Wahabari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP) na Jumuiya ya Misitu Kimataifa (CFI) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo