NHIF kutumia wiki ya utumishi wa umma kutoa elimu
NA SAIDA ISSA, DODOMA
Akizungumza kwenye viwanja vya maadhimisho hayo jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa NHIF, James Mlowe (pichani), alisema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo limeendelea kuwa changamoto kubwa kwa sekta ya afya.
“Kwa sasa, zaidi ya asilimia 60 ya gharama zote za matibabu tunayolipa kila mwaka zinahusiana na magonjwa yasiyoambukiza,Kwa mfano, mwaka uliopita NHIF ilitumia takribani shilingi bilioni 700 kwa ajili ya huduma kwa wanachama wake”, alisema.
Aidha Mlowe alisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na maradhi hayo, akisema juhudi hizo zitasaidia kupunguza gharama kubwa za matibabu na kuruhusu fedha kuelekezwa katika kuboresha huduma nyingine za afya.
Aliongeza kuwa NHIF imeongeza kasi ya mageuzi ya kidijitali kupitia mfumo wa 'NHIF Jihudumie', unaowezesha wanachama kujihudumia kupitia simu zao za mkononi kupitia mfumo huu ambapo mwanachama anaweza kujisajili, kuangalia taarifa za michango, kuongeza wategemezi na kupata kadi ya bima bila kufika ofisi za NHIF.
“Mwanachama sasa anaweza kutumia kadi ya kidigitali kupata huduma katika vituo zaidi ya 10,000 vilivyosajiliwa na NHIF nchi nzima,Hii ni hatua kubwa katika kupunguza msongamano na kuimarisha ufanisi wa huduma”, aliongeza.
alisema pia kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayohimiza matumizi ya teknolojia katika sekta ya umma, NHIF imeeleza kuwa mwelekeo huo ni chachu ya kuwafikia wananchi wengi kwa haraka na kwa njia rahisi.
Mlowe pia alieleza kuwa kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023, NHIF sasa imefungua milango kwa wananchi wote, wakiwemo watoto na wajasiriamali, kwa kutumia vifurushi kama Toto Afya Kadi na Tarangire, ambavyo vinapatikana kupitia mfumo wa Jihudumie.
Kwa ujumla, NHIF inatilia mkazo elimu, teknolojia na upanuzi wa huduma ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya huduma bora za afya.
“Katika maadhimisho haya, tunajielekeza kutoa elimu na huduma bora kwa kila mmoja. Huu ni wakati wa kuwekeza zaidi kwenye kinga kabla ya tiba”, alisema Mlowe.
Comments
Post a Comment