Majaliwa awawashia moto watendaji wanaodaiwa 'kukwapua' mamilioni

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa (pichani) amewasimamisha kazi mkaguzi Mkuu, Mkaguzi Msaidizi na baadhi ya watendaji wa wizara ya Fedha na Mipango ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zinazowakabili.

Alichukua hatua hiyo katika kikao kazi na waziri wa Fedha na Mipango, Kaibu Mkuu, Manaibu  Katibu Wakuu na Watendaji Waandamizi wa Wizara hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

 

Mbali ya hatua hiyo, Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kamishna wa Polisi, CP Salum Rashid Hamdun kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikithibitika kwamba tuhuma si za kweli wahusika watarejeshwa kazini.

 

Majaliwa alizitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni malipo yaliyofanyika Machi 31, mwaka huu  kupitia vocha 30 ya shilingi milioni 251 yakielezwa kuwa ni malipo maalum bila kutaja kazi hiyo maalum ni kazi gani na nani aliifanya hiyo kazi.

 

Alisema  siku hiyo hiyo  ya Machi 31 pia zililipwa  shilingi milioni 198.8 kwa madai kuwa ni posho ya honoraria.

 

Majaliwa  alisema Aprili 8 mwaka huu watumishi 27 wa  wizara hiyo walilipwa shilingi milioni 44.5 zikiwa ni posho ya kazi maalum ya wiki nne. Pia Aprili 13 mwaka huu zililipwa shilingi milioni 155.2 kwa watumishi 68 ikiwa ni posho ya kazi maalum ya wiki tatu.

 

Aidha, Aprili 30 mwaka huu zililipwa shilingi milioni 43.9 kwa ajili ya kuandaa  mpango wa kuhifadhi mazingira na siku hiyo hiyo zililipwa shilingi milioni 14.4 kwa ajili ya siku ya wanawake. Fedha nyingine shilingi milioni 43 zililipwa siku hiyo na kufanya  jumla ya malipo yaliyolipwa siku hiyo kuwa shilingi milioni 101.8.

 

Alisema kuwa, Mei mosi mwaka huu zililipwa shilingi shilingi milioni 184.1 na mchana zililipwa shilingi milioni 264 zikiwa ni malipo ya kazi maalum. "Sisi tulikuwa Mwanza tunasherehekea siku ya wafanyakazi duniani nyinyi hapa ndani mnalipana posho”,alisema.

 

Aliongeza kuwa Mei 3 mwaka huu zililipwa shilingi milioni 146.5 kwa  watumishi 125 zikiwa ni malipo ya kuandaa mpango kazi wa manunuzi kazi ambayo  ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku, ambapo tarehe hiyo hiyo zililipwa  shilingi milioni 171.2 kwa ajili ya kuandaa nyaraka za Bunge.

 

Majaliwa  alisema shilingi milioni 155 zililipwa kwa baadhi ya watumishi zikiwa ni posho ya kuandaa miongozo ya kazi. " Yaani hii kazi ya ukaguzi imelipwa kwenye  maeneo manne, huu ni utaratibu wa wapi? Mnazidi kutupunguzia imani,  na sijaongea eneo la kuhamisha mafungu na utaratibu wa kuhamisha fedha  kisha mnakwenda kuzichukuwa huko mlikozihamishia."

 

Majaliwa aliwataka watendaji wa wizara hiyo kujenga uaminifu kwa wanaokusanya mapato kwa kufanya kazi kwa uaminifu na alitahadharisha kuwa watakaoendekea kucheza na pesa za umma hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

 

Aidha, waziri mkuu aliwapongeza watendaji wengine wa wizara hiyo ambao wameendelea kufanya kazi kwa weledi “na nimesema hapa si wote wenzenu wachache wanatumia vibaya nafasi zao kutuchafua wizara ya fedha”.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango