Othman akutana na balozi wa Uingereza, Mwakilishi UNICEF

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imekubali kufanya kazi na Serikali ya Uingereza katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kidunia, likiwemo suala la dawa za kulevya kwa lengo la kuendelea kuilinda Zanzibar na watu wake.

Othman amesema hayo alipofanya mazungumzo na Msaidizi Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Rick Shearn, wakati Balozi huyo alipofika kwa ajili ya kujitambulisha kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ofisini kwake Migombani, mjini Unguja.

Balozi Shearn ameonesha azma ya serikali ya Uingereza kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye masuala kadhaa, likiwemo hilo la kupambana na uhalifu unaovuuka mipaka ya mataifa.

Alisema bado kuna mambo yanaendelea kuiumiza dunia hasa suala la madawa ya kulevya na ufichwaji wa fedha za kihalifu.

“Serikali imekubaliana kupitia vyombo mbalimbali vinavyohusika na usimamizi wa sheria, uchunguzi, usimamizi wa kodi pamoja na vile vinavyosimamia maeneo makuu ya kuingia Zanzibar, kufanya kazi pamoja na Uingereza kwa lengo la kudhibiti uhalifu huu wa kidunia,“ alisema Othman.

Aidha othman, aliongeza kwamba Balozi Shearn ameahidi kutoa ushirikiano katika kuvijengea uwezo vyombo hivyo pamoja na kutanua wigo wa ushirikiano na vyombo vya kimataifa.

Sambamba na hilo, Uingereza imeahidi pia kuongeza nguvu ili kuboresha uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Wakati huo huo, Othman alikutana na muwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Shalin Bahugana, ambaye ameihakikishia Serikali ya Zanzibar mashirikiano ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inaendelea kuwa vyema katika masuala mbali mbali ya kiafya na maisha kwa vijana wake.

Mwakilishi huyo alisema wamejipanga kuja na mkakati maalum wa kuwasaidia vijana kutokana na changamoto za kimaisha na za kiuchumi kwa kutoa taaluma juu ya kujenga maisha yao.

“Sisi katika UNICEF tumeandaa mpango mkubwa kuhusiana na utoaji wa taaluma juu ya lishe bora, jambo ambalo limekuwa tatizo kwa wananchi walio wengi kujisimamia katika suala zima la ulaji, na hivyo kupelekea kukosa jamii iliyo bora,“ alisema Bahugana.

Kwa upande wake, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia mwakilishi huyo wa UNICEF kuwa serikali itaendelea kuungana nao pamoja katika kuhakikisha jamii ya Zanzibar inakuwa na ustawi mzuri, hasa katika suala la afya.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango