Miradi 93 yasajiliwa siku 100 za Samia

NA MWANDISHI MAALUM, OWM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha siku 100 za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imesajili miradi 93 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.6 itakayozalisha ajira 24,600.

Alisema kuwa hatua hiyo inatoa alama kwa wawekezaji wa nje kwamba kwa sasa urasimu katika sekta ya uwekezaji unaendelea kupunguzwa katika maeneo ya usajili wa makampuni pindi muwekezaji anapokusudia kuja kuwekeza nchini.

Waziri Mkuu aliyasema hayo Juni 27,2021 alipofungua kongamano la siku 100 za Rais Samia lililofanyika katika kituo cha mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Alisema mbali na miradi hiyo, pia serikali ya Rais Samia amefanya jitihada kubwa ya kuondoa tozo 232 zilizokuwa zinawakwaza wafanyabishara ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao nchini.

“…Na haya yote ni katika kuongeza mzunguko wa fedha kwa Watanzania ambao wanashiriki katika shuhguli mbalimbali za kuimarisha uchumi wao,” alisema Mjaliwa. 

Waziri Mkuu alisema katika kufanya kazi zake, Rais Samia ameendeleza mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi jirani ambapo ametembelea nchi za Kenya, Uganda na Msumbiji kwa lengo la kuimarisha urafiki na Mataifa ya jirani.

Majaliwa aliongeza kwamba Samia ameendelea kupanga mipango ya ujenzi wa miradi mipya katika siku 100 za uongozi wake ikiwemo kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kimataifa kipande cha kutoka Mwanza mpaka Isaka, ujenzi wa meli mpya nne na ukarabati wa meli kongwe moja.

"Meli hizi zimewekwa katika maeneo yote, ziwa Victoria tuna meli moja ambayo ina uwezo wa kubeba tani 3000 za mizigo itakayotoa huduma kati ya Tanzania, Kenya na Uganda, pia meli nyingine ya MV Umoja ambayo awali ilikuwa inakwenda Uganda nayo inakarabatiwa," alisema.

Aidha alisema katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa serikali imeanzisha mradi wa shule za sekondari za wasichana katika halmashauri zote nchini na imetoa shilingi milioni 500 kwa kila jimbo kwa ajili ya ukarabati wa barabara ili kuuimarisha huduma za usafiri vijijini.

Akizungumza katika kongamano hilo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi, alisema kuwa katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais Samia mamlaka hiyo imepokea barua za pongezi kutoka katika makampuni makubwa ya usafirishaji duniani ikiwemo ya Mediterrainian na Mesina Line kwa uboreshaji wa huduma bandarini hapo.

Alisema kuwa katika kipindi cha robo ya mwisho kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu wameweza kukusanya shilingi bilioni 236.8 sawa na ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na robo iliyopita ya kuanzia Januari hadi Machi ambayo walikusanya shilingi bilioni 203.

Nae, Kamishna wa Uhamiaji nchini, Dkt. Anna Makakala alisema kwa kushirikiana na idara ya kazi wameanza kutoa vibali kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ambapo katika kipindi cha kuanzia Mei 2021 hadi sasa wametoa vibali 3,377 vya kazi ukilinganisha na vibali 2,166 vilivyotolewa katika kipindi kama hiki kwa mwaka jana.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango