Wanahabari waombwa kuhamasisha chanjo ya UVIKO 19
NA ASYA HASSAN
MENEJA Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kutokana Wizara ya Afya Zanzibar, Bakar Hamad Magarawa, amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kuendelea kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya ya UVIKO - 19.
Alisema
hayo alipokuwa akiwasilisha mada katika mkutano wa mafunzo kwa waandishi wa
habari juu ya hali halisi ya maradhi hayo na upatikanaji wa chanjo yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) kwa
kushirikiana na Internews.
Alisema
lengo la serikali hadi kufika Disemba mwaka huu asilimia 70 ya wananchi wawe
tayari wamechanjwa lakini hadi sasa waliochanjwa ni asilimia 35, hali inayoonesha
kwamba kuna kundi kubwa halijahamasika kupata kinga hiyo.
Sambamba na
hayo alifahamisha kwamba licha ya serikali na waandishi wa habari kufanya kazi
kubwa ya kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuchanja bado jamii haijaona
umuhimu huo.
Alisema kwa
sasa vipo vituo zaidi ya 120 vinavyotoa chanjo hizo katika maeneo mbalimbali, hivyo
aliiomba jamii ikavitumia ipasavyo ili kupata chanjo hiyo.
Alisema tokea
walipoanza kutoa chanjo hiyo, watu 267,824 sawa na asilimia hiyo 35.10
wamechanjwa, hivyo aliwaomba waandishi wa Habari kuendelea kuhamasisha.
“Tunashukuru
kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari lakini bado tuendelee kwani wapo watu
wengi hawajajitokeza hivyo ipo haja ya kuendeleza kupatiwa elimu,” alieleza
Magarawa.
Akitaja
miongoni mwa sababu zinazochangia jamii kutokubali kupata chanjo ni pamoja na
dhana kwamba chanjo inapunguza nguvu za kiume, kukosa uzazi kwa wanawake na
baadhi ya watu kuamini kwamba chanjo hizo zinasababisha watu kugeuka wanyama.
Aidha
alifahamisha kwamba serikali zote mbili zimefanya uchunguzi na kubaini kwamba
chanjo hizo ni salama, hivyo alitumia fursa hiyo kuihamasisha jamii kukubali
kupata kinga.
“Serikali imeandaa
miongozo mbali mbali ili kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kupata chanjo na
mambo mengine, hivyo ni vyema wananchi kwenda sambamba na mikakati ya serikali
ili kuweza kuwa na afya bora,” aliongeza Meneja huyo.
Aidha Magarawa aliitaka jamii kuelewa kwamba ugonjwa huo bado upo na kwamba wagonjwa
wanaendelea kupokelewa ambapo hadi Agosti 25, 2022 kulikuwa na wagonjwa watano
katika hospitali ya Mnazimmoja ambao baadhi yao ni watalii na wengine ni
wasafiri waliongia nchini kutoka nje ya nchi.
Akiwasilisha
mada ya uandishi wa habari za UVIKO 19 na chanjo dhidi ya ugonjwa huo, Mkuu wa Idara
ya mafunzo Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma Zanzibar ya chuo Kikuu cha
Taifa Zanzibar (SUZA) Imane Duwe, aliwataka waandishi kuchukua tahadhari pale
wanapokuwa katika majukumu yao ili wajikinge na maradhi hayo.
Kwa upande
wa Mwanasheria na Mwandishi wa Habari wa Shirika la Magazeti ya Serikali, Juma
Khamis Juma, alisema ugonjwa wa UVIKO - 19 uliathiri kwa kiasi kikubwa
upatikanaji wa habari na uhuru wa kujieleza.
Juma alieleza
hayo alipokuwa akiwasilisha mada katika mafunzo hayo na kueleza kuwa hali hiyo
ilisababisha waandishi wa habari kufanya kazi katika mazingira magumu na wakati
mwengine kunyimwa taarifa muhimu zinazohusiana na ugonjwa huo.
Alisema baadhi
ya vikwazo vimeondoka na kutoa rai kwa waandishi wa habari kuendelea
kuihamasisha jamii kupata chanjo kwa sababu kwa sasa upatikanaji wa chanjo hiyo
umerahisishwa.
Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa ZPC, Abdalla Abdulrahman Mfaume, aliwataka waandishi kuyatumia mafunzo hayo ili yalete tija katika kazi zao.
Aliongeza kuwa
ZPC kwa kushirikiana na wadau mbali mbali itaendelea kuchukua juhudi za
kuwapatia mafunzo wanachama na waandishi wa Habari ili kuimarisha kazi zao.
Awali akitoa
taarifa kuhusu mafunzo hayo, Katibu wa ZPC, Mwinyimvua Nzukwi, alieleza kuwa
mafunzo hayo yalilenga kuwakumbusha wandishi wa habari na jamii juu ya umuhimu wa kuchukua
tahadhari dhidi ya UVIKO 19.
Aidha Nzukwi alieleza kuwa ugonjwa huo umeanza kuzoeleka kiasi cha watu kuacha kuchukua tahadhari na kutochukua hatua zinazoelekezwa na wataalamu wa afya hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuwakumbusha ili iendelee kuwa salama.
Comments
Post a Comment