Mchakato ujenzi kituo cha biashara, mikutano kimataifa waanza

NA MWANDISHI WETU

WIZARA ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imeeleza kuwa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa uwanja wa maonesho ya biashara ya kimataifa na kituo cha mkutano na hoteli, kutaimarisha uchumi wa Zanzibar.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji wa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa uwanja wa maoenesho ya biashara na kituo cha mikutano kimtaifa katika ofisi za wizara hiyo Kinazini, Waziri, Omar Said Shaaban wa wizara hiyo alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake kibiashara.

Alieleza kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo kunakwenda kutekeleza ndoto za Zanzibar kuwa na kumbi za mikutano za kimataifa zinazoweza kuchukua idadi kubwa ya watu na vifaa vya kisasa kutekeleza dhana ya uchumi wa buluu.

Alisema kuwa ukumbi huo pamoja na hoteli ya kisasa vitajengwa Mbweni wakati kituo cha maonesho ya biashara kitakachojengwa Nyamanzi, wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, kinalenga kusisimua biashara na kuirudisha Zanzibar kuwa kitovu cha biashara.

Akizungumza kwa niaba ya kampuni ya Elsewedy, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ukanda wa Afrika Mashariki, Mhandisi Ibrahim Qamar alieleza kufurahishwa na hatua hiyo ambayo ni matokeo utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano yaliyofanywa na kampuni mbali mbali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, mjini Dubai.

“Wakati wa maonesho ya Dubai mapema mwaka huu, kampuni kadhaa zilitia saini makubaliano na Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi kadhaa, sisi (Elsewedy Electric) tuliamua kuja Zanzibar kuanza uwekezaji kwenye maeneo haya mawili, kama tulivyofanya Tanzania bara,” alieleza Mhandisi Qamar.

Alifafanua kwamba makubaliano hayo yanahusu upembuzi yakinifu, usanifu, uhandisi, ununuzi na kazi za ujenzi kwa miradi yote miwili kazi ambayo itafadhiwa kampuni hiyo na kutekelezwa katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.

“Tunaamini kazi hii itakamilika ndani ya muda ili tuanze kazi kubwa zaidi ambayo tunaamini kwa mashirikiano tunayoyapata kutoka wizarani tutafanikisha ndoto za serikali na kampuni yetu ambayo imewekeza sehemu mbali mbali Afrika,” alileza Mhandisi Qamar.

Alieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa wakati kabla ya kukubaliana namna ya kutekeleza ujenzi wa miradi hiyo inayokadiriwa kutumia zaidi ya dola milioni 100 za marekani.


Waziri Omar Said Shaaban (kushoto), akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Elsewedy ukanda wa Afrika Mashariki, Mhandisi Ibrahim Qamar. 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango