TMA kujenga vituo saba vya rada

NA SAIDA ISSA, DODOMA

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 imejipanga kujenga vituo vya rada saba pamoja na vifaa vitakavyosaidia kuangaza nchi masaa 24.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dodoma, Mkurugenzi Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa, kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2022/23 amesema kuwa licha ya kuanzisha miradi hiyo, wataalamu wamepatiwa mafunzo  kwa ajili ya kuendesha rada hizo.

“Mafunzo kwa wahandisi na waendesha mitambo kuhusu kuzihudumia na kuzitumia rada hizo yalifanyika kiwandani nchini Marekani. Aidha utengenezaji wa rada mbili za mwisho zitakazofungwa KIA (uwanja wa ndege wa kimataifa Kilimanjaro) na Dodoma ulifikia asilimia 45 ambapo mamlaka ilifungua barua ya dhamana kwa ajili ya malipo ya asilimia 80 ya utengenezaji wa Rada hizo,” amesema Dk. Kabelwa.

Alifafanua kwamba kukamilika kwa rada hizi kutakamilisha mtandao wa rada nchini kufikia saba rada ambazo zina uwezo wa kuona zaidi ya kilomita za mkato 450 huku zikizunguka na kuona matone madogo sana ya mvua katika hali ya uhalisia ndani ya kilometa 250.

Akizungumzia mikakati ya mamlaka hiyo Dk. Kabelwa amesema mamalaka hiyo imejipanga kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau wengine juu ya umuhimu wa huduma za hali ya hewa na kuendelea na utekelezaji wa Sheria Na.2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake.

“Tumedhamiria kuimarisha uangazi wa hali ya hewa katika bahari na maziwa makuu ili kuimarisha usalama wa abiria wa kwenye maji, shughuli za uvuvi pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali zikiwemo upakuaji wa mizigo bandarini na uvunaji wa gesi asilia,” amefafanua.

Ameongeza kuwa; “Tumejipanga kufanya ufuatiliaji kwa wakandarasi wanaotengeneza Rada na vifaa vya hali ya hewa ili vikamilike na kuwasili nchini na kuhakikisha wadau wote wenye vifaa vya hali ya hewa nchini wanavifunga vifaa hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 na Kanuni zake”.

Aidha amesema mpango mwingine ni kuongeza vyanzo vya mapato kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa, kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na kuandaa miradi yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

Ameongeza kuwa  TMA inaendelea na juhudi za kuongeza mapato kwa kuwafikia wadau wake na kuwaeleza juu ya umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa ambapo amesema Jitihada  zimepelekea mapato ya Mamlaka kuongezeka kwa asilimia 53% katika mwaka wa fedha 2021/22.

Hata hivyo Dk. Kabelwa amesema mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya tafsiri ya taarifa zinazotolewa na watu mbali mbali ambazo hazina usahihi juu ya masuala ya hali hewa na vipindi vya mvua hapa nchini.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango