NMB, ATCL waja na 'Anga rafiki - Tiketi yako imebima'

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAM

BENKI ya NMB na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamezindua ushirikiano wa kibiashara wa malipo ya tiketi za ndege ujulikanao kama 'Anga Rafiki - Tiketi Yako Imebima'.

AFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi wakionesha mfano wa ndege kuashiria uzinduzi wa mfumo wa malipo ya tiketi za ndege kupitia matawi na mawakala wa NMB  hafla iliyofanyika jijini Dar es salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa ATCL, Jamal Kiggundu na kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.

Mfumo huo unaowapa fursa wasafiri watakaotumia ndege za shirika hilo kulipia tiketi kupitia matawi, mawakala na huduma za NMB Mkononi (NMB app) ambazo zitakuwa zimekatiwa bima ya safari.

Ushirikiano huo umezinduliwa jana katika Makao Makuu ya NMB jijini Dar es salaam ambapo Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth Zaipuna, alieleza kuwa msafiri atakayelipia tiketi za safari za ndani ya nchi kupitia NMB, atakatiwa bima ya maisha, ulemavu ama upotevu wa mizigo safarini, ambapo atalipwa hadi shilingi Milioni tano 5 za Kitanzania itapotokea mteja kufariki dunia.

Alieleza kuwa huduma hiyo itapatikana kupitia matawi 229 na mawakala zaidi ya 21,000 hatua inayopelekea wasafiri kufikiwa kirahisi na kuweza kupata tiketi na kwamba wateja wa benki hiyo wanazo njia za ziada za kulipia tiketi hizo kwa simu ya mkononi.

"Ni imani yetu kwamba, huduma hii sio tu inaenda kumpa urahisi na wepesi msafiri wa kulipia tiketi yake, bali kumkinga pia na majanga yatokanayo na safari kama ulemavu, kifo na upotevu wa mizigo”, alieleza Zaipuna.

Aliongeza kuwa iwapo mzigo wa msafiri utapotea, mteja wetu atalipwa shilingi 300,000, lakini safari itasogezwa ama kuakhirishwa, atalipwa shilingi 150,000 za bima kupitia washirika wa NMB kampuni ya Reliance Insurance.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, aliipongeza NMB kwa ushirikiano huo wa kuweka ziada ya Bima ya Safari kwa wateja wao, huku akibainisha kwamba hakuna tena sababu ya Watanzania kusafiri kwa hofu wakati kuna ATCL na NMB.

"ATCL kila siku tumejikita katika kuboresha utoaji huduma zetu, kuanzia tiketi inapokatwa, mteja anapokuwa safarini hadi kufika, hivyo tunajivunia ushirikiano wetu na NMB, ambao unaenda kututofautisha na watoa huduma za usafiri wa anga wengine waliopo sokoni.

"Ni ushirikiano unaoenda kumaliza kabisa hofu ya upatikanaji tiketi za safari na usalama wa abiria wetu na mali zao wawapo safarini hii ni kutokana na ziada zilizowekwa na NMB kwa abiria watakaolipia kupitia mtandao wao mpana wa matawi, mawakala na huduma za NMB Mkononi kama alivyotangulia kusema CEO Zaipuna," aliongeza Matindi.

Aidha Matindi aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uwezeshaji inaowapa katika kutoa huduma kwenye sekta ya usafiri wa anga kitaifa na kimataifa ambapo kufikia mapema mwakani mtandao wa ndege za shirika hilo zitafikia 16.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango