Zaipuna awapa msukumo vijana kuikabili changamoto za karne ya 21

NA MWANDISHI WETU

AFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amewashauri vijana nchini kunoa ujuzi wao wa karne ya 21 ili kufanikiwa katika soko la kisasa la ajira lenye ushindani.

Akizungumza katika mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne wa skuli za sekondari za Feza yaliyofanyika jijini Dar es salam mwishoni mwa wiki, Zaipuna alisema ujuzi wa Karne ya 21 ni pamoja na kufikiri kwa kina, ubunifu, ushirikiano, mawasiliano, tekinolojia ya habari, uongozi, na stadi za maisha.

“Mkiwa na ujuzi huu, nina hakika kabisa kwamba mtafaulu katika shughuli zenu za maisha iwe mnataka kuajiriwa au kujiajiri. Mtawavutia waajiri na wawekezaji na kwa moyo wa kuendelea kujifunza, mtaimarika siku hadi siku na kujiongezea thamani,” Zaipuna alisema.

Aliongeza, “Kwa miaka mingi, nimekuwa sehemu ya Shule za Feza na ninathamini sana msisitizo ambao shule inaweka katika elimu ya maisha na maendeleo, ushirikiano na jamii na ukuzaji wa stadi za uongozi, sifa ambazo naamini zitakuwa na athiri chanya kwa watoto wetu kwa miaka mingi ijayo”, alisema.

Aidha Zaipuna alibainisha kuwa maisha ni safari na kuwataka vijana hao kufanya kazi kwa bidii na kuongeza kuwa wanaweza kufikia chochote wanachokusudia endapo wataendelea kuwa na nidhamu.

“Nilianza safari yangu takriban miongo mitano iliyopita. Miaka 32 iliyopita, nilihitimu kidato cha nne katika Skuli Sekondari Kilakala, Morogoro. Siku hii imenifanya kutafakari maisha yangu yote tangu nilipohitimu mwaka 1991”, alisema.

Hivyo aliwataka wanafunzi hao kujiamini, kufuata nafsi zao na kamwe wasipoteze maadili na kanuni walizopandikizwa wakiwa shuleni.

Alibainisha kuwa baadhi ya vitu ambavyo vimesaidia kupanda daraja la mafanikio ni pamoja na nidhamu, bidii, uadilifu, ubora katika kila kazi iwe kubwa au ndogo na kuendelea kujifunza mambo mbalimbali.

 “Licha ya vikwazo ambavyo mmekumbana navyo mkiwa hapa, mmeibuka kuwa nyota zinazongaa. Katika miaka yenu yote katika Shule za Feza, mmeonyesha dhamira isiyoyumba kwa kuendela kufanya vyema. Mafanikio haya ni uthibitisho wa bidii zenu", alisema.

Aliwashauri wahitimu hao kuchangamkia fursa zinazowajia huku akiongeza kuwa mafanikio hayapimwi kwa alama au sifa tu, bali pia kwa matokeo yanayopatikana katika maisha ya wengine.

Awali, Naibu Mkurugenzi wa Shule za Feza, Ali Nungu, aliwataka wahitimu kuendeleza miiko ya shule hiyo ilikuleta mabadiliko katika njia watakayochagua.

Aliwapongeza walimu wa shule hiyo, wafanyakazi wengine na wazazi ambao walichukua jukumu kubwa katika safari ya wahatimu hao na kuwataka wahitimu kuamini katika uwezo wao.

Alionyesha imani kwamba kwa tabia zao nzuri, uwezo bora wa kitaaluma na ustahimilivu, watakuwa wakakamavu na wenye shauku katika kutimiza ndoto zao.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango