AfDB kuendelea kukuza uchumi wa Tanzania

NA BENNY MWAIPAJA, DODOMA

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, amefanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dk. Kevin Kariuki na kuishukuru benki hiyo kwa kufadhili miradi 29 ya kitaifa na kikanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.84

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (kulia) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dk. Kevin Kariuki walipokutana kwa mazungumzo jijini Dodoma.

Mazungumzo baina ya wawili hao yamefanyika jijini Dodoma ambapo Dk. Nchemba amesema kuwa AfDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo huku katika miradi hiyo, miradi 26 ni ya kitaifa na mitatu ni ya kikanda iliyopo katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati, maji na kilimo. 

Amesema kuwa zaidi ya asilimia 13.6 ya fedha hizo zimeelekezwa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme kupitia miradi mitano ambapo mitatu kati ya hiyo ni ya kitaifa na mingine miwili ni ya kikanda inayolenga kuunganisha umeme katika nchi za Afrika Mashariki.


Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dk. Kevin Kariuki (kushoto), akieleza nia ya Benki yake kuendelea kusadia maendeleo ya Tanzania na kuunga mkono juhudi za serikali za kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba. Kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dk. Patricia Raverley.

Dk. Nchemba, aliitaja miradi hiyo kuwa ni  Mradi wa Umeme wa Mto Malagarasi (49.5 MW), Kakono (87.8 MW), Gridi ya kaskazini Magharibi (400 KV), Maporomoko ya Maji Rusumo (80 MW) na utakaounganisha nchi za Burundi, Rwanda na Tanzania pamoja na mradi wa umeme unaoziunganisha Kenya na Tanzania.

Pia Dk. Nchemba alibainisha kuwa AfDB imekubali kushiriki katika Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) wa Kikanda wenye lengo la kuunganisha huduma za usafiri na usafirishaji abiria na mizigo kati ya Tanzania nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo mikataba ya mkopo huo nafuu itasainiwa hivi karibuni.


Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dk. Patricia Raverley, akizungumza wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dk. Kevin Kariuki (kushoto), uliofanyika jijini Dodoma. 

Aidha liiomba Benki hiyo kusaidia utekelezaji wa mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Katika mazungumzo yao, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayesimamia masuala ya Nishati, Dk. Kevin Kariuki, aliahidi kuwa Benki yake ipo tayari kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza katika Nishati safi ya kupikia, kuendelea kufadhili miradi ya ujenzi wa miudombinu ya usambazaji umeme, kilimo na maji.


Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (kushoto), akiwa katika mkutano na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dk. Kevin Kariuki (kulia) uliojadili fursa za uwekezaji katika sekta mbali mbali uliofanyika jijini Dodoma.

Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano kwa kupigania matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiongozwa na Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuwa Benki yake itamuunga mkono ili kufanikisha mradi huo.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Kevin Kariuki, ambaye ni raia wa Kenya, aliambatana na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dk. Patricia Raverley.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (wa sita toka kulia) na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Nishati, Dk. Kevin Kariuki (wa saba toka kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania na AfDB baada ya kumalizika mkutano kati ya pande mbili hizo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha).

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango