Wadau kuujadili uhuru wa habari Zanzibar
NA MWANDISHI WETU
KAMATI ya maandalizi ya siku ya uhuru wa habari duniani Zanzibar, imeeleza kuwa maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani yanategemewa kufanyika Mei 23, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo inayoundwa na Baraza la habari Tanzania (MCT ) Ofisi ya Zanzibar , Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA - ZNZ), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA) na Klabu ya Waandishi wa Wabari Zanzibar (ZPC), Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Mzuri Issa, alisema maadhimisho hayo yatafanyika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Zanzibar.
Alisema maadhimisho hayo yatahudhuriwa pamoja na waandishi wa habari, wadau mbali mbali wa habari na wawakilishi kutoka asasi za kiraia za ndani ya Zanzibar.
Dk. Mzuri alisema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba ujumbe wa ‘Uhuru wa vyombo vya habari na mageuzi ya sera na sheria za habari Zanzibar’ ambao ni muhimu katika kukuza na kuimarisha kada ya habari nchini na kutoa wito maalum kwa wadau wa habari kuhusu umuhimu wa kuwa na sera na sheria rafiki zitakazoongeza ufanisi wa utendaji kazi wa vyombo vya habari.
Aidha alisema shughuli hiyo itaambatana na majadiliano katika mada mbali mbali zenye lengo la kuimarisha na kukuza kada ya habari hapa nchini.
Alifahamisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatatanguliwa na shughuli za kukuza na kuimarisha kada ya habari ikiwemo kuandaa vipindi vya masuala ya uhuru wa habari, mikutano na mafunzo kwa waandishi wa habari katika masuala ya sheria za habari.
“Nia ya shughuli hizo ni kukuza weledi na umahiri wa waandishi wa habari katika masuala ya sheria za habari ili watumie kalamu zao katika kufanya uchechemuzi wa sheria hizo”, alisema.
dk. mzuri alieleza pia mijadala itahusu mafanikio na changamoto, wapi tunatoka na upi mwelekeo wa kukuza na kuimarisha kada ya habari hasa ikizingatiwa umuhimu wa sekta ya habari katika kuleta maendeleo na kuibua kero za wananchi.
Alisema kuwa uandishi wa habari ni kada muhimu katika kukuza na kuendeleza demokrasia, uwazi na uwajibikaji hivyo waandishi hao hawana budi kuwa na sheria nzuri za habari ili ziweze kuwalinda katika kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu.
Alieleza kuwa suala la kuwa na sheria nzuri za habari hapa nchini pia litajadiliwa katika mjadala huo ambalo muda mrefu limekuwa likizungumzwa na wadau wa habari, ambapo hadi hivi sasa kuna Sheria ya Usajili wa Mawakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Namba 5 ya 1988 na marekebisho yake mwaka 1997, na sheria ya Tume ya Utangazaji Namba 7 ya mwaka 1997 na marekebisho yake ya mwaka 2010.
Alisema suala la kuwa na sheria mpya na nzuri ya habari limekuwa katika mchakato na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa katika kukusanya maoni ya wadau hivyo Mswada huo umeshirikisha fikra na maoni tofauti.
Aidha masuala ya jinsia na vyombo vya habari yatakuwa na nafasi ya kipekee ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha masuala ya jinsia katika vyombo vya habari ili haki na usawa katika vyombo vya habari iweze kuimarishwa.
Comments
Post a Comment