POSTA TANZANIA YATUNUKIWA CHETI CHA USALAMA NA UPU
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Posta Tanzania limetunukiwa Cheti cha Usalama cha Kimataifa (S58 & S59) kutoka Umoja wa Posta Duniani (UPU), kufuatia mafanikio katika zoezi la tathmini ya usalama wa mifumo, miundombinu na taratibu za utoaji huduma lililokamilika Novemba 7, 2025.
Katika zoezi hilo, Shirika la Posta Tanzania limepata alama 598 kati ya 640, likitimiza kwa ufanisi vigezo vyote vya kupewa cheti hicho cha heshima kinachotolewa kwa taasisi za posta zinazofikia viwango vya juu vya usalama wa kimataifa.
Wakipokea cheti hicho, Caroline Kanuti kwa niaba ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Ndani ya Shirika, S.P. Mathias Kipeta, wameishukuru UPU kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Shirika katika kuimarisha usalama wa huduma zake na kuahidi kuendeleza maboresho endelevu katika mifumo na miundombinu ya Shirika.
Aidha wataalamu
wa UPU waliwasilisha mapendekezo ya kuongeza ufanisi zaidi katika maeneo ya
udhibiti wa mizigo, ufuatiliaji wa usafirishaji wa barua na vifurushi na uimarishaji
wa vituo vya kuchakata mizigo (Office of Exchange) ili kuhakikisha huduma bora,
salama na za kisasa.
Kupitia mafanikio
hayo, Posta Tanzania sasa imeorodheshwa rasmi miongoni mwa waendeshaji wa
huduma za posta duniani waliotunukiwa cheti cha usalama na UPU hatua
inayoliweka shirika katika nafasi ya juu kimataifa na kuimarisha uaminifu,
ushindani na ubora wa huduma kwa wananchi na wateja wa kimataifa.



Comments
Post a Comment