Absa Tanzania yahamasisha wajasiriamali kutumia huduma za kifedha

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya Absa Tanzania imeendelea kuhamasisha wanawake wajasiriamali kutumia huduma rasmi za kifedha ili kuimarisha biashara zao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za benki hiyo katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia huduma zinazolenga kuongeza ujuzi wa usimamizi wa fedha, upatikanaji wa mitaji na matumizi ya teknolojia katika biashara.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani jijini Dar es Salaam, ambayo Absa ilikuwa miongoni mwa wadau waliodhamini, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa benki hiyo, Victor Nchimbi, alisema benki hiyo inatambua mchango mkubwa wa wajasiriamali katika kukuza uchumi.

MKUU wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Victor Nchimbi, akizungumza na wajasiriamali kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo zinazowalenga wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani ambapo Absa ilikuwa moja ya taasisi zilizojitokeza kudhamini tukio hilo, jijini Dar es salaam hivi karibuni.

Alisema kupitia akaunti maalumu ya SHE, benki hiyo imeweka huduma zinazolenga kuwawezesha wanawake wajasiriamali kuendesha biashara zao kwa urahisi na ufanisi zaidi.

Alieleza kuwa akaunti hiyo haina makato ya kila mwezi ya uendeshaji, ina ada nafuu za miamala na inawawezesha watumiaji kufanya miamala kwa fedha za Tanzania pamoja na fedha za kigeni.

"Tunatambua mchango wa wajasiriamali Tanzania, hususan wanawake, ndiyo maana tumeendelea kuweka huduma mbalimbali ikiwemo mikopo yenye gharama nafuu, huduma za kidigitali na akaunti ya SHE inayolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi," alisema Nchimbi.

MENEJA Bidhaa wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Devroda Kagusa (kulia) akizungumza kuhusu huduma za benki hiyo zinazowalenga wafanyabiashara wadogo na wa kati, kwa baadhi ya wahudhuriaji wa Maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani.

Aliongeza kuwa kupitia huduma hiyo, wanawake wajasiriamali pia hupata mafunzo yanayowasaidia kuboresha uendeshaji wa biashara, kupanga matumizi ya fedha na kukuza shughuli zao.

Kwa upande wake, mmoja wa wajasiriamali anayejishughulisha na biashara ya vipodozi, Maua Jumanne, alisema changamoto kubwa inayowakabili wanawake wengi ni ukosefu wa elimu ya fedha, mitaji na maarifa ya kuendesha biashara kwa ufanisi.

MENEJA Bidhaa wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Devroda Kagusa (kulia) akizungumza na wafanyabiashara wadogo na wa kati, kwa baadhi ya wajasiriamali waliofika katika   Maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani, yaliyowakutanisha zaidi ya wajasiriamali 350, viongozi wa sekta, na watunga sera chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Alizitaka taasisi za kifedha kuendelea kuwafikia wajasiriamali wadogo na kuwapatia elimu ya mikopo na usimamizi wa biashara ili kuwawezesha kukuza mitaji yao na kutoa wito kwa benki kuwafikia wajasiriamali wadogo na kuwapa elimu ya namna ya kupata mitaji na kutumia mikopo kwa maendeleo ya biashara zetu.

Alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa baadhi ya wajasiriamali kwa mikopo isiyo rasmi yenye gharama kubwa na kuwawezesha kukuza biashara zao kwa mazingira salama.

OFISA Huduma kwa Wateja wa Benki ya Absa, Mboni Sabura (katikati) akizungumza na baadhi ya wajasiriamali  kuhusu huduma ya akaunti maalumu ya wanawake ya SHE wakati wa  Maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani yaliyofanyika  jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani
huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kutambua nafasi ya wajasiriamali katika kukuza uchumi, kuunda ajira na kuibua ubunifu unaochochea maendeleo ya jamii.

Siku hiyo pia hutumika kuhamasisha mazingira bora ya biashara, upatikanaji wa mitaji, elimu ya ujasiriamali na sera zinazowawezesha wajasiriamali wadogo na wakubwa kufikia malengo yao.

 

BAADHI ya Wawezeshaji na Wajasiriamali walioshiriki Maadhimisho ya Siku ya Wajasiriamali Duniani wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilika kwa maadhimisho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni ambapo benki ya Absa ilikuwa moja ya taasisi zilizojitokeza kudhamini tukio hilo.


Comments

Popular posts from this blog

'Zanzibar Matibabu Card' yashinda tuzo ya WSIS

Vyombo vya habari vinapaswa kusimamia mshikamano wa Afrika - UAJ