Uwazi matumizi ya bahari nyenzo muhimu kulinda uchumi wa Afrika – Tony Long
NA MWANDISHI WETU
Long alisema kwa karne nyingi jamii za pwani ya mashariki mwa Afrika zimeitumia Bahari ya Hindi kama chanzo cha biashara, ajira na maendeleo, huku akieleza kuwa umuhimu wa bahari unaendelea kuongezeka wakati ambapo uchumi wa buluu unatajwa kuwa miongoni mwa nguzo kuu za maendeleo ya bara.
Alisema sekta za uvuvi na ufugaji wa samaki huchangia takribani dola bilioni 24 za Marekani kila mwaka katika uchumi wa Afrika, wakati thamani ya uchumi wa buluu wa bara hilo ikikadiriwa kufikia dola bilioni 300.
Hata hivyo, Long alisema ukuaji huo unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kukosekana kwa uwazi katika shughuli nyingi za uvuvi wa baharini.
Akinukuu matokeo ya utafiti wa mwaka 2024 uliofanywa na Global Fishing Watch na kuchapishwa katika jarida la Nature, alisema takribani asilimia 75 ya shughuli za uvuvi wa viwandani duniani hazionekani katika mifumo ya wazi ya ufuatiliaji.
Alisema hali hiyo inatoa mwanya kwa uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa unaoendelea kupunguza rasilimali za bahari, kudhoofisha wavuvi wanaofuata sheria na kupunguza mapato ya serikali.
“Uwazi unamaanisha kujua nani anamiliki vyombo vya uvuvi, vinafanya kazi wapi, vina vibali gani na kama vinafuata sheria zilizowekwa”, alisema Long.
Alifafanua kuwa matumizi ya mifumo ya kisasa kama Automatic Identification System (AIS) na Vessel Monitoring System (VMS), pamoja na picha za satelaiti na uchambuzi wa data, yanawezesha mamlaka kupata taarifa sahihi za shughuli za baharini na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria.
Aidha, alisema teknolojia pekee haitoshi bila kuwepo kwa dhamira ya kisiasa, ushirikiano wa kimataifa na sera zinazohimiza uwazi katika usimamizi wa rasilimali za bahari.
Long alisema hatua ya nchi 11 kupitisha Azimio la Mombasa wakati wa Mkutano wa 11 wa Our Ocean Conference ni ishara ya kujitolea kuimarisha uwazi kupitia usajili wa vyombo vya baharini, uchapishaji wa vibali vya uvuvi na kuboresha ushirikiano wa kubadilishana taarifa.
Alisisitiza kuwa kwa nchi za Afrika zikiwemo Tanzania na Zanzibar, uwazi katika shughuli za baharini utasaidia kupambana na uvuvi haramu, kulinda uchumi wa buluu, kuongeza mapato ya serikali na kuhakikisha rasilimali za bahari zinawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Comments
Post a Comment