Hemed azindua programu ya malezi, makuzi ya awali ya mtoto
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imezindua Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto pamoja na Kituo cha Kulelea Watoto katika Soko la Mwanakwerekwe, ikiwa ni hatua ya kuimarisha ustawi wa watoto na kuwawezesha wazazi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Akizindua programu hiyo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, alisema Serikali inaamini kuwa uwekezaji katika malezi na makuzi ya awali ya mtoto ni msingi wa kujenga taifa lenye afya, elimu bora na uchumi imara.
Alisema programu hiyo itawaunganisha wazazi na walezi katika kupata huduma muhimu zinazohusu afya, lishe, ulinzi na maendeleo ya watoto tangu wakiwa wadogo.
Hemed alisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya malezi kwa kuanzisha vituo vya kulelea watoto katika masoko, hospitali na skuli za awali ili kuwawezesha wazazi kutekeleza majukumu yao bila kuwa na hofu kuhusu usalama wa watoto wao.
Alisisitiza kuwa kituo hicho si jengo pekee bali ni uwekezaji kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo akaitaka jamii na wadau kuhakikisha kinatunzwa ili kiendelee kutoa huduma bora.Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Atanas Poul, alisema Serikali itapanua huduma za vituo vya kulelea watoto kuanzia ngazi ya shehia hadi mkoa ili kuhakikisha watoto wanapata malezi salama na bora.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema mafanikio ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar yanategemea uwekezaji katika mtoto, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Serikali, washirika wa maendeleo, taasisi, wazazi na walezi katika utekelezaji wa programu hiyo.




Comments
Post a Comment