Programu kuimarisha elimu Chaani yazinduliwa

Waziri Lela asema itaongeza hamasa ya kujifunza 

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa, amesema programu ya kuimarisha elimu katika jimbo la Chaani itapunguza changamoto zinazowakabili wazazi na walezi katika kugharamia mahitaji ya wanafunzi, hususani gharama za kambi za masomo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika katika viwanja vya Skuli ya Chaani Masingini, alisema Serikali ya awamu ya nane inaendelea kuitanguliza sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu, kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia katika ngazi zote.

WAZIRI Lela,  Mbunge na Mwakilishi wa jimbo la Chaani wakikabidhi moja ya makoksi ya karatasi kwa mmoja ya walimu wakuu skuli za jimbo kwa ajili ya mitihani ya kujiandaa na mitihani ya taifa  ya wanafunzi wa skuli zao.

Alisema dhamira hiyo inaonekana kupitia ongezeko la bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ambapo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga zaidi ya shilingi trilioni 1.1, sawa na ongezeko la asilimia 27.3 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka uliopita.

Lela alisema programu hiyo itawanufaisha zaidi ya wanafunzi 600 wa darasa la saba na kidato cha nne kutoka skuli zote za jimbo hilo kupitia kambi maalumu za kujiandaa na mitihani ya kitaifa

Alieleza kuwa utekelezaji wa programu hiyo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za kijamii na wananchi katika kuboresha elimu na kuwaandaa wanafunzi kufaulu mitihani na kutimiza ndoto zao.

Alisema vifaa vya kujifunzia vilivyotolewa vitawasaidia wanafunzi kuongeza maarifa, kukuza uwezo wa kujisomea na kujiandaa vizuri kwa maisha yao ya baadaye.

WAZIRI Lela,  Mbunge wa jimbo la Chaani wakikabidhi fedha kwa viongozi wa kamati za maendeleo ya skuli za jimbo kwa ajili ya kambi za wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya taifa na maendeleo ya kitaluma ya skuli zao.

Aidha, alisema Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Chaani, Serikali ya Mkoa, taasisi ya Mimi na Wewe Foundation na wadau wengine wa maendeleo kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, zikiwemo uchakavu wa miundombinu, uhaba wa madarasa, vyoo, walimu, maktaba na huduma za mtandao.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Tanzania, Ayoub Mohamed, alisema uongozi wa jimbo umejipanga kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa ya kusoma bila vikwazo vinavyotokana na gharama za elimu.

Alisema viongozi wa jimbo watahakikisha chakula kinapatikana katika kambi za masomo kwa wakati, walimu wanapatiwa usafiri na wanafunzi wenye uhitaji wanasaidiwa kupata viatu ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao.

WAZIRI Lela,  Mbunge na Mwakilishi wa jimbo la Chaani na viongozi wengine wakikagua baadhi ya viti mwendo kabla ya kukabidhiwa kwa wananfunzi wenye ulemavu.

"Nitahakikisha wananchi wa Jimbo la Chaani wanapata maendeleo bila ubaguzi wa chama au dini, huku tukitoa kipaumbele kwa elimu kama msingi wa maendeleo ya jamii," alisema Ayoub.

Aidha, aliiomba Serikali kuanzisha elimu ya Kidato cha Tano na Sita katika jimbo hilo pamoja na kujenga jengo la ghorofa kwa ajili ya kuongeza nafasi za kujifunzia kutokana na ongezeko la wanafunzi.

Nae Mwakilishi wa Jimbo wa jimbo hilo, Juma Usonge Hamad, alisema programu hiyo itapunguza gharama za uendeshaji wa kambi za masomo, ikiwemo chakula na usafiri wa walimu, hatua itakayochangia kuimarisha ufaulu wa wanafunzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ame, aliwataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao na kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na elimu.


WAZIRI Lela akipokea zawadi toka kwa wenyeji wake Mbunge na Mwakilishi wa jimbo la Chaani.

Nao baadhi ya wazazi na walezi waliipongeza Serikali pamoja na viongozi hao kwa kuanzisha programu hiyo, wakisema itaondoa mzigo wa gharama za maandalizi ya mitihani na kuongeza ari ya wanafunzi kujifunza.

Katika uzinduzi huo, viongozi wa jimbo walikabidhi tani 25 za mchele, magodoro, vifaa vya kujifunzia, taulo za kike, baiskeli kwa wanafunzi wenye ulemavu pamoja na mafuta kwa ajili ya kuendesha shughuli za kambi za masomo kwa ajili ya skuli 12 za msingi na sekondari za jimbo hilo.

Comments

Popular posts from this blog

Vyombo vya habari vinapaswa kusimamia mshikamano wa Afrika - UAJ

'Zanzibar Matibabu Card' yashinda tuzo ya WSIS